
OFISI ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetoa ufafanuzi juu uwepo wa upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea katika Mikoa yote Nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Pia ofisi imekemea vikali vitendo vya watu ambao siyo waaminifu ambao wanapotosha na kusababisha taaruki au kuomba rushwa kwa walimu ambao wanatafuta ajira jambo ambalo ni kinyume na taratibu ya ajira.
Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini Lynn Chawala inasema kuwa
kutokana na upotoshaji unaoendelea kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea katika Mikoa yote nchini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeona upo umuhimu wa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.
Chawala ameeleza kuwa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kama sehemu
ya utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, kifungu cha (4.2)(ii)(iii) inayoelekeza kuwa ajiira za ushindani zifanyike katika madaraja ya kuingilia kwenye miundo ya utumishi na kiundwe chombo cha ajira katika Utumishi wa Umma kitakachokuwa kinashughulikia na kusimamia upatikanaji wa wataalamu mbalimbali.
Akifafanu suala hilo amesema katika kuwezesha utekelezaji wa Sera hii, Kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, kinaelekeza kuwepo kwa chombo maalumu cha kushughulikia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.
Amesema kuwa Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2021 zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na.580 la Mwaka 2022 ndizo zinazozingatiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023, kifungu cha (3.12.1.5) inaelekeza kuwa: Serikali itaimarisha mfumo wa ajira ya walimu, wakufunzi, na wahadhiri kwa kuhakikisha kuwa wenye sifa na viwango stahiki wanaajiriwa baada ya kufanya mitihani na kufaulu kama sehemu ya usaili”imeeleza taarifa hiyo.
Kuhusu lengo la kuanzishwa kwa Sekretarieti ya ajira taarifa inaeleza kuwa lengo kuu la kuundwa kwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni kuziwezesha Mamlaka za Ajira kupata nafasi ya kutekeleza majukumu yao ya msingi kama yalivyoainishwa katika miongozo ya uanzishwaji wa Taasisi hizo (Instruments).
MCHAKATO WA AJIRA UNAVYORATIBIWA
Taarifa inasema kuwa Mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma huendeshwa na Sekretarieti ya Ajira kwa niaba ya mamlaka za ajira katika Utumishi wa Umma zinazojumuisha: Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali; Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma.
“Sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeweka bayana mipaka ya majukumu ambapo, ajira zote zinazohusu,Mhimili wa Bunge, Mhimili wa Mahakama,na vyombo vya ulinzi na usalama zinaendelea kusimamiwa na mihimili na taasisi hizo na hivyo kutoihusisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
“Vile vile, Kifungu cha 29(A) (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma ili kukidhi mahitaji ya Serikali, kimempa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira uwezo wa kukasimu madaraka kwa Afisa Mtendaji Mkuu au kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuendesha mchakato wa ajira.
“Pia, Sheria inampa uwezo Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuchukua majukumu aliyoyakasimu kwa taasisi nyingine kadiri atakavyoona inafaa.
“Kwa sasa, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma amezikasimu madaraka ya kuratibu mchakato wa ajira taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BOT); Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kada 23; pamoja na vyuo Vikuu vya Umma kwa kada za wanataaluma.”imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa imezitaja taratibu nyingine kuwa ni pamoja na Utoaji wa matangazo ya ajira,utaratibu wa kupokea maombi ya ajira,utaratibu wa kuchakata maombi ya ajira,utaratibu wa usaili,kukasimisha Mamlaka ya kuajiri kwa baadhi ya Wizara na Taasisi na usajili wa kada za walimu.
Kwa kukamilisha ufafanuzi huo Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Utumishi wa Umma imeeleza kuwa inawasihi watu wote wanaotafuta fursa za ajira katika Utumishi wa Umma wenye sifa stahiki wakiwemo walimu, kujiandaa vizuri kabla ya usaili, kujiamini na kushiriki katika usaili ili waweze kufaulu na kupangiwa vituo vya kazi kadiri nafasi za ajira zinapojitokeza.
“Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawahakikishia waombaji fursa za ajira kuwa mchakato wa ajira chini ya ofisi hii unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi bila ya rushwa wala upendeleo wowote.
“Vilevile, kama wadau wetu muhimu tunawaomba mtupatie taarifa kila mtakapobaini upungufu wowote vikiwemo vitendo visivyo vya kimaadili ili sisi wenyewe kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali tuweze kuchukua hatua stahiki kwa wakati pamoja na kuboresha zaidi huduma zetu”taarifa imejieleza kutipia kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini LynnChawala.
ZINAZOFANANA
Serikali imeondoa tozo kwa wanufaika wa mikono, kulipa madeni pekee
Uboreshaji wa mitaala mpya elimu wawakosha wana Dodoma
Jafo ataka watanzania wachamkie fursa za AGOA, azindua Bodi ya Uongozi wa CBE