
SHIRIKISHO la Viwanda Tanzania (CTI) liliendesha warsha na wadau mbalimbali kujadili changamoto kubwa la unywaji wa pombe haramu na hatarishi kwa binadamu unaoendelea hivi sasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Warsha hiyo iliwaunganisha wadau muhimu wa sekta ya viwanda, watunga sera, na mamlaka za udhibiti kama Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na wadau wengine muhimu katika sekta ya pombe.
CTI ilisisitiza hatari kubwa za kiafya zinazotokana na pombe zisizodhibitiwa, ikiwa ni pamoja na viwango vya juu vya sumu, madhara ya muda mrefu kama ugonjwa wa ini, upofu, na hata vifo. Aidha, pombe haramu inachangia matatizo ya kijamii kama uhalifu, unyanyasaji wa majumbani, na kushuka kwa ufanisi kazini, hali inayoongeza mzigo kwa mifumo ya afya na ustawi wa jamii.

Mwenyekiti wa zamani wa CTI, Paul Makanza, alisema, “Mapambano dhidi ya pombe haramu si tu suala la udhibiti—ni juhudi za kulinda maisha ya Watanzania, kulinda mapato ya serikali, na kuendeleza mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki. Pombe haramu inahatarisha afya ya umma, inachochea matatizo ya kijamii, na inadhoofisha sekta rasmi ambayo inatoa maelfu ya ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi. Tunahitaji kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera huku tukiendelea kuongeza uelewa ili kuhakikisha sekta ya pombe inayowajibika na endelevu ambayo inachangia maendeleo ya Tanzania kwa njia chanya.”
Akiunga mkono maoni ya Mwenyekiti wa zamani, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, aliongeza: “Sisi, kama wazalishaji wa pombe, tuko tayari kushirikiana katika jitihada hizi. Tunaamini kuwa mafanikio ya kweli katika sekta hii hayapimwi tu kwa utendaji wa kifedha, bali pia kwa uwezo wetu wa kuchangia maendeleo endelevu ya jamii yetu. Matumizi mabaya ya pombe ni hatari kwa kila mtu—sekta, afya ya umma, na jamii—na kushughulikia changamoto hii kunahitaji ushirikiano.”

Mbali na athari za kiafya, CTI ilielezea wasiwasi wake juu ya athari za kiuchumi zinazotokana na pombe haramu. Utafiti uliofanywa na Ernest & Young mnamo Novemba 2018 ulibaini kuwa serikali ya Tanzania inapoteza takriban shilingi trilioni 1.2 kila mwaka kutokana na biashara ya pombe haramu. Mauzo yasiyodhibitiwa yanadhoofisha biashara halali na kusababisha hasara kubwa ya mapato ya kodi, hali inayopunguza uwezo wa serikali kufadhili huduma muhimu kama afya na elimu. Zaidi ya hayo, sekta rasmi ya pombe—ambayo inatoa maelfu ya ajira—inakabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka kwa waendeshaji wasiosajiliwa ambao wanakwepa kanuni za usalama na viwango vya ubora.
Ili kulinda afya ya umma na uthabiti wa uchumi, CTI ilitoa wito wa udhibiti mkali wa sekta ya pombe, ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha imani ya wawekezaji, kuhamasisha unywaji wa pombe kwa uwajibikaji, na kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa hatari.
CTI na washirika wake wanatoa wito kwa serikali na wadau kuongeza juhudi za kupambana na pombe haramu kupitia utekelezaji madhubuti wa sheria, kuongeza uelewa wa umma, na kuboresha utekelezaji wa sera. Ushirikiano kati ya viongozi wa sekta, mamlaka za udhibiti, na vyombo vya usalama ni muhimu ili kuhakikisha sekta salama na yenye uwajibikaji katika unywaji pombe inayosaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.
ZINAZOFANANA
Vodacom Foundation kufadhili kongamano la Utafiti wa Elimu Tanzania 2025
Samia: Uhitaji wa kahawa duniani ni fursa kwa Afrika
SBL yazindua kampeni ya SMASHED kukabiliana na unywaji wa pombe chini ya umri