![](https://mwanahalisionline.com/wp-content/uploads/2025/02/GjfKZ4KX0AAW73X.jpg)
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Pindi Chana amefungua rasmi Onesho la wiki ya wabunifu wa Italia kituo cha Makumbusho ya Taifa jijini Dar es salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hafla ya ufunguzi huo imefanyika tarehe 10 Februari, 2025 usiku, ambapo onesho hilo linatarajiwa kufanyika mpaka tarehe 20 Februari 2025, linaloonesha picha za wabunifu mbalimbali wakubwa wa zamani kutoka nchini Italia.
Dk. Chana amepongeza nchi hiyo kwa ushirikiano kati yake na Tanzania kwenye sekta ya utalii. ameiomba Italia kuwekeza kwa vijana wa Kitanzania kwa kuunga mkono juhudi zao za ubunifu ili kutengeneza mustakabali wao ambapo Tanzania na Italia zinasherehekewa katika soko la kimataifa.
Waziri Chana amesema “Nchi yetu sio tu kitovu cha utalii bali pia ni shamba la uvumbuzi na ubunifu. Vijana wa Kitanzania wamejaa vipaji, na kwa usaidizi na uwekezaji unaofaa, wanaweza kuchukua nafasi yao miongoni mwa wabunifu na wavumbuzi wakuu duniani.”
“Italia imejitolea katika juhudi zetu za kukuza utalii endelevu na kuhifadhi urithi wetu wa asili na kiutamaduni .Mfano mmoja mzuri wa ushirikiano huu ni mradi wa Kisiwa cha Bawe, ambao ni mwanzo mzuri unaoonyesha utalii endelevu. Mradi huu hauangazii tu uzuri wa visiwa vya Tanzania bali pia unaonesha matokeo chanya ya uwekezaji wa kigeni katika uchumi wetu.” amesisitiza Chana.
Aidha, amesema kuwa katika kuendeleza mahusiano hayo Tanzania na Italia zinatarajiwa kuwa na Kongamano la Biashara na Uwekezaji katika siku mbili zijazo, jijini Dar es Salaam ambalo ni jukwaa la mazungumzo, ushirikiano, na litatoa matokeo yenye manufaa kwa mataifa yetu yote mawili.
ZINAZOFANANA
Usalama mtandaoni ni amani kwa Taifa
Dk. Mpango mgeni rasmi kikao kazi cha Serikali mtandao
mapambano dhidi ya biashara haramu ya maliasili yazidi kuimarishwa