September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bei mafuta ya petrol, dizeli yapaa Agosti

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA), imetangaza bei mpya za mafuta ya petrol na dizeli ya rejareja ambazo zinaonesha kupanda katika mikoa inayochukua mafuta hayo kwenye bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …  (endelea)

Kwa mujibu wa EWURA, bei za bidhaa hiyo zitakazotumika kuanzia leo tarehe 7 Agosti 2024, zimeongezeka kwa asilimia 6.3 huku ile ya dizeli ikiongezeka kwa asilimia 2.2.

Watumiaji wa nishati ya petroli katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, sasa watalazimika kulipia Sh 3,231 kwa lita ya petroli na Sh 3,131 kwa dizeli, kwa mwezi Agosti.

“Gharama za bidhaa za mafuta zinajumuisha bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji ambazo ni gharama za usafirishaji, bima na gharama na faida za mleta mafuta kabla ya kodi, tozo na gharama nyingine za hapa nchini,” imesema EWURA katika taarifa yake kwa umma.

Kwa mujibu wa mdhibiti huyo, gharama ya mafuta yanayopokelewa na gharama za uagizaji zinalipiwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani na sarafu za nchi nyingine.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.

Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

About The Author