February 7, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bwawa la Kidunda kuimarisha upatikanaji wa maji Dar es Salaam

 

UJENZI wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika Jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani. Mradi huo, unaogharimu takribani shilingi bilioni 336, umefikia asilimia 27 ya utekelezaji wake, huku ukitarajiwa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 190 za maji. Anaripoti Yusuph Kayanda, Morogoro … (endelea).

Kwa mujibu wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Bwire Mkama, bwawa hilo litasaidia kupunguza uhaba wa maji, hasa wakati wa kiangazi. Akizungumza katika ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) walipotembelea eneo la mradi, alisema utekelezaji wake ni hatua muhimu kwa ustawi wa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani.

Meneja wa Mazingira na Uratibu wa Jumuiya za Watumia Maji kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu, Janeth Kisoma, alieleza kuwa bwawa hilo ni miongoni mwa vyanzo vya maji vinavyosimamiwa na bodi hiyo, na mipango inaendelea kulifanya eneo hilo kuwa tengefu kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa maji.

Katika jitihada za kulinda mazingira ya mto Ruvu, Janeth alibainisha kuwa bodi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejenga zaidi ya mabirika 29 ya kunyweshea mifugo katika vijiji vinavyozunguka mto huo. Hatua hiyo inalenga kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha mifugo haiingii mtoni moja kwa moja, ikiwa ni sehemu ya mpango wa uhifadhi wa maji kupitia kaulimbiu ya “Tone la maji lazima lihifadhiwe.”

About The Author

error: Content is protected !!