BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imehitimisha rasmi kampeni yake ya ’Shinda mechi zako Kinamna yako’ kwa kukabidhi zawadi ya gari ya pili aina BMW X1 kwa Galus Peter Casto maruufu kama “Kweka” ambae ni mfanyabiashara mdogo ‘Machinga’ kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es salaama alieibuka mshindi wa zawadi hiyo kuu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kampeni hiyo iliyolenga kuchochea ukuaji wa uchumi miongoni mwa wateja wa benki hiyo kupitia uwekaji wa akiba, ilizinduliwa April mwaka jana ambapo pamoja na kutoa gari aina BMW X1 mbili kwa washindi wakuu pia ilitoa fursa kwa wateja hao kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, simu za mikononi, ‘laptops’, friji, ‘tablets’ za watoto, bima za afya pamoja na majiko ya kisasa ya kupikia.
Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo imefanyika mapema leo kwenye tawi la Benki ya NBC Soko la Kariakoo ikiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki hiyo Bw Joseph Lyuba pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo akiwemo Meneja wa tawi hilo, Mohamed Tegalila.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hiyo Lyuba pamoja na kuwapongeza wateja waliofanikiwa kuibuka washindi wa zawadi mbalimbali za kampeni hiyo akiwemo Kweka, alisema kampeni hiyo iliyodumu kwa miezi 10 imehitimishwa kwa mafanikio makubwa kufuatia muitikio ilioupata kutoka kwa wateja kupitia uwekaji akiba.
“Pamoja na kukabidhi zawadi mbalimbali kwa wateja wetu zikiwemo gari hizi mbili, mafanikio ya kampeni hii yanathibitishwa kupitia ufikiwaji wa lengo letu kuu la kampeni hii ambalo ni kuchochea kasi ya watanzania katika kujiwekea akiba. Kupitia kampeni hii tumeweza kuwafikia Watanzania wa makundi yote kiumri na kiuchumi na hiyo ndio sababu mshindi wetu wa gari hii ya pili ametoka kwenye kundi la wafanyabiashara wadogo kupitia akaunti yake ya Malengo,’’ alibainisha.
Kwa mujibu wa Lyuba jumla ya zawadi zenye thamani ya Sh. 200 milioni zimetolewa kwa washindi mbalimbali wa kampeni hiyo tangu kuanzishwa kwake.
“Zaidi ya aina 8 ya zawadi zilizotolewa kupitia kampeni hii zilikuwa zipo kimkakati zaidi tukilenga ziwasaidie wateja wetu kwenye kufanikisha majukumu yao kiuchumi ambayo ndio maana hali ya ‘Shinda mechi zako’ zikiwemo nyenzo za biashara na vitendea kazi vitakavyoweza kuwarahisishia kazi zao,’’ aliongeza
Akiizungumzia zaidi kampeni hiyo Meneja Masoko wa Benki hiyo, Alina Kimaryo alisema ilihusisha wateja wote waliokidhi vigezo na masharti na wanaohudumiwa na benki hiyo kupitia huduma zake mbalimbali zikiwemo akaunti za Chanua, Akaunti ya Malengo, Akaunti ya Mwalimu pamoja na akaunti ya Johari.
“Mwisho wa kampeni hii ni mwanzo wa ujio wa kampeni nyingine nyingi kutoka NBC lengo ni kuunga mkono nia ya serikali ya kuchochea uchumi jumuishi kupitia uwekaji akiba kwenye taasisi rasmi za kifedha. Naendelea kuwasihi Watanzania wenzangu hususani vijana waendelee kutumia vema fursa za kampeni hizi ili waweze kunufaika kupitia malengo yake yaani kujiweka akiba huku pia wakiwa kwenye nafasi ya kujishidia zawadi mbalimbali’’ alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Kariakoo, Mohamed Tegalila alisema ushindi wa mteja huyo ambae ni mfanyabiashara mdogo kutoka Kariakoo ni uthibitisho tosha kuwa uwepo wa benki hiyo kwenye soko hilo umekuwa kimbilio kubwa kwa wafanyabiashara katika eneo hilo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa zawadi yake, Kweka alieambatana na mke wake Bi Miriamu Kweka, pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa makabidhiano hayo alisema ushindi huo umetokana na yeye kujiwekea akiba kupitia akaunti ya malengo kwa ajili ya ada za watoto wake lengo ambalo alifanikiwa kulitimiza.
“Nashukuru pamoja na kufanikiwa kulipa ada za watoto wangu kupitia akaunti ya malengo pia nimefanikiwa kupata zawadi ya gari litakalonisaidia kuwafikia zaidi wateja wangu huko mitaani. Nashukuru kwa kuwa zawadi hii itanirahisishia ‘Kushinda mechi zangu’’, alisema Kweka. Kauli hiyo iliungwa mkono na mkewe ambae alitoa wito kwa wanawake wenzie nchini kuendelea kuwamasisha waume zao kujiwekea akiba kwenye taasisi rasmi za kifedha.
Akithibitisha uhalali wa kampeni hiyo Balozi wa Benki ya NBC, Conrad Kennedy, maarifu kwa jina ‘Coy Mzungu’ alisema pamoja na kushuhudia uendeshwaji wa droo mbalimbali za kampeni hiyo pia alishuhudia uwepo wa maafisa wa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania hatua iliyozidisha uwazi katika upatikanaji wa washindi hao.
ZINAZOFANANA
Mali za magendo zitakazokamatwa nchini kutaifishwa
Meridianbet yawashika mkono Magomeni Makuti
Meridianbet yaonyesha ukuaji wake kwenye kikao cha mwisho wa mwaka