
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea na tathmni ya uwepo wa magugu maji katika Ziwa Victoria ili kupatia ufumbuzi changamoto hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Januari 31, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Constantine John Kanyasu aliyetaka kujua kama Serikali inafahamu ongezeko la magugu maji katika Ziwa Victoria, zipi ni athari za magugu hayo na mpango wa kuyadhibiti.
Amesema Serikali imechukua jitihada za kudhibiti magugu maji katika ziwa hilo ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa na kutekeleza Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka 2019-2029 ambao unatoa mwongozo wa namna ya kuzuia kuingia na kuenea kwa viumbe vamizi na una mipango endelevu ya kushughulikia viumbe vamizi waliopo na wale wanaoweza kuingia.
“Spika, tathmnini inaendelea na nimuombe mbunge avute subira wakati tunaendelea kulishughulikia jambo hili kwani limeendelea kuathiri vyanzo vingi vya maji nchini kwa mfano Ziwa Jipe nalo lina changamoto ya kuzingirwa na maji,” amesema Khamis.
Ameongeza kuwa Serikali inawajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na ziwa kuhusu namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza na kuenea kwa magugu maji kila yanapojitokeza ikiwemo kung’oa, kukausha na kuchoma magugu maji na kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kudhibiti uharibifu mifumo ikolojia ya Ziwa Victoria.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis amesema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 imeweka msisitizo kwa miradi yote mikubwa ni lazima ifanyiwe tathmini ya awali ya athari za mazingira kabla ya mradi kuanza ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
Amesema Sheria pia inahimiza wananchi kuhamasishwa kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kupitia elimu, sheria ndogo za serikali za mitaa, na mipango ya hifadhi ya mazingira.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Ernest Nollo aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuweka Sheria Kabambe kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.
Amefafanua kuwa Sheria hii imeweka msisitizo wa udhibiti wa uharibifu wa mazingira kwa kukataza uchafuzi wa maji, hewa, na udongo kupitia kemikali za viwandani, kilimo, na shughuli nyingine za binadamu.
Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis ameriarifu Bunge kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji imetenga fedha shilingi bilioni 1.08 kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa la Kalemawe lililopo katika Wilaya Same mkoani Kilimanjaro.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Naghenjwa Livingstone Kaboyoka aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa tope lililojaa katika Bwawa la Kalemawe – Same, Khamis amesema ukarabati umepangwa kufanyika katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Ametaja shughuli zinzotarajiwa kufanyika ni pamja na kukamilisha kazi ya usanifu wa kina na kuandaa gharama kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo kwa kuondoa tope, kukarabati utoro wa maji, kujenga msingi wa tuta na tuta la bwawa.
Duh!
Kwa maneno bila data hujajibu swali. Na hoja ya viumbe vamizi haina data.