MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema msimu wa mvua za masika zinatarajiwa kuanza Machi 2025 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, hasa Kanda ya Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini, na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akitoa taarifa hiyo leo Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dk. Ladislaus Chang’a amesema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Pwani ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa Victoria, na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Ameongeza kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na maeneo ya mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.
Amesema mwelekeo wa mvua za masika 2025 kwa Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani zitaanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Machi na kuisha wiki ya kwanza ya mwezi Mei.
Aidha mikoa ya Pwani ya Kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba) inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani ambazo zitaanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Machi na kumalizika wiki ya tatu hadi ya nne ya mwezi Mei.
Pia Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani ambapo zitaanza wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi Machi na kumalizika wiki ya kwanza mwezi Mei.
Amesema athari zinazotarajiwa ni pamoja na unyevu na mafuriko, ambapo mvua nyingi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo, na huenda zikapelekea mafuriko na kuathiri ukuaji wa mazao.
Amesema kuhusu maji, kina cha maji katika mito na mabwawa kinaweza kuongezeka na hivyo hatari ya mafuriko inaweza kujitokeza.
Pia magonjwa ya mlipuko yanaweza kutokea kutokana na uchafuzi wa maji unaoweza kusababisha magonjwa hayo.
Amesisitiza kuwa taarifa hiyo inatolewa kwa ajili ya kusaidia wadau wa sekta mbalimbali, kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili, afya, nishati, usafirishaji na usimamizi wa maafa, kuchukua tahadhari stahiki na kupanga mikakati ya kukabiliana na athari za mvua.
Awali alisema mwenendo wa mvua za msimu wa mwaka (Novemba 2024 – Aprili 2025) zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma, huku mvua za wastani hadi juu ya wastani zikitarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, Lindi na mikoa mingine kusini.
Hata hivyo amesema taarifa hiyo inatoa mwanga wa jinsi mifumo ya hali ya hewa itakavyokuwa kwa maeneo mbalimbali, kusaidia wahusika kupanga na kufanya maamuzi bora.
ZINAZOFANANA
Majaliwa: Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa TMA
Waziri Jafo akagua maandalizi miaka 60 ya CBE
TRA, Wafanyabiashara Kariakoo kufanya Bonanza la pamoja J’pili