December 12, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

RC Kunenge Aridhishwa na Jitihada Nishati Safi Mkoani Pwani, Aipongeza Taifa Gas

 

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameonyesha kuridhishwa na jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali mkoani humo ikiwemo kampuni ya Taifa Gas katika kufanikisha kampeni ya mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo taasisi za elimu na wafanyabiashara wa vyakula. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri wa mkoa kilichofanyika ofisini kwake mwishoni mwa wiki, RC Kunenge pamoja na kutambua jitihada za Taifa Gas katika kufanikisha kampeni hiyo aliwataka viongozi mbalimbali mkoani humo kushirikiana kwa ukaribu na wadau hao ili kuhakikisha taasisi na migahawa inakidhi viwango vya nishati safi ndani ya muda uliowekwa.

Akiweka mkazo juu ya mchango wa Taifa Gas, RC Kunenge alielezea jinsi kampuni hiyo ilivyojizatiti kuwezesha shule na wauzaji wa vyakula kuhamasika katika kutumia nishati ya gesi ya kupikia (LPG) kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Kijamii (CSR).

“Kama ilivyo kwa wadau wengine, Taifa Gas imekuwa mshirika muaminifu katika safari hii. Shule za Sekondari za wasichana za Ruvu na Bibi Titi zimefaidika sana kupitia jitihada zao, ambapo Sekondari ya Wasichana ya Ruvu imepata miundombinu ya nishati ya gesi ya kupikia (LPG) na matenki bure.’’ Alisema RC Kunenge huku akibainisha kuwa Sekondari ya Wasichana ya Bibi Titi inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Zaidi, RC Kunenge alitaja mabadiliko yaliyofanyika miongoni mwa wauzaji wa vyakula mkoani humo ambapo kwa sasa wengi wao wanatumia nishati ya mitungi ya gesi (LPG) ambayo imetolewa na Taifa Gas. “Mabadiliko haya yameonekana pia kuwanufaisha sana wafanyabiashara wetu wa vyakula kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi. Tunathamini sana juhudi hizi za Taifa Gas,” aliongeza.

Akizungumzia mafanikio hayo Meneja Mahusiano wa Taifa Gas, Bi Angela Bhoke alisema kwa kiasi kikubwa yamechagizwa na muitikio wa kampuni hiyo katika kuunga mkono kampeni ya matumizi ya nishati ya kupikia iliyoasisiwa na Rais Dk Samia mwaka 2022.

“Kupitia hamasa hiyo Taifa Gas imeongoza mfululizo wa jitihada mbalimbali katika kufanikisha nia hiyo ya Rais Dkt Samia ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa kampeni yetu ya utunzaji wa mazingira kupitia matumizi ya nishati safi hususani katika mkoa huu wa Pwani,’’ alisema.

Alisema kupitia kampeni hiyo, kampuni hiyo ilifanikiwa kuhamasisha manispaa hiyo katika uhifadhi wa mazingira na uelewa wa nishati safi ya kupikia kupitia gesi (LPG) na hivyo kuchochea hatua kubwa kama vile kuzuia usafirishaji wa mkaa kuingia Dar es Salaam kwa pikipiki na kupunguza vibali vya kuvuna misitu vinavyotolewa na mamlaka za mitaa.

“Mafanikio ya kampeni hiyo yametuwezesha kuimarisha juhudi zetu katika mikoa mingine, ikiwemo Dar es Salaam na Morogoro, tukiwa na dhamira thabiti ya kuunga mkono ajenda ya upishi safi ya Rais Dkt Samia. Hivyo, ushuhuda wa RC Kunenge unadhihirisha mafanikio ya Taifa Gas katika kukuza uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, na kufanya tofauti halisi katika jamii mbalimbali nchini Tanzania,’’ alihitimisha.

About The Author

error: Content is protected !!