WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana (Mb) ameweka jiwe la misingi la ujenzi wa mradi wa miundombinu ya Ngorongoro Lengai Geopark wenye thamani ya Sh. 25 bilioni unaofadhiliwa Serikali ya China kwa lengo la kuongeza zao la utalii wa Jiolojia nchini (Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark). Anaripoti Mwandishi Wetu, Karatu, Arusha … (endelea).
Hafla hiyo imefanyika Karatu, Mkoani Arusha, leo Novemba 16, 2024 ambapo Dk. Chana amesema ujenzi wa makumbusho hiyo ushuhuda wa maono ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika ukuaji wa sekta ya utalii na uhifadhi wa mazingira hapa nchini.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema utekelezaji wa mradi huo unatokana na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China na ndio unaoleta matokeo ya kuboresha miundombinu ikiwemo sekta ya utalii.
‘‘Ushirikiano kati ya Tanzania na China umeimarika vya kutosha na niwahakikishie kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania kusaidia ujenzi wa miradi mbalimbali hususan katika maendeleo ya sekta ya utalii,” amesema Chen.
Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dk. Elirehema Doriye amesema kuwa Mradi wa makumbusho hiyo wenye hadhi ya viwango vya dunia utakapokamilika, utasaidia watalii kutoka mataifa mbalimbali kufurahia zao la utalii wa miamba kutokana na vivutio vitakavyokuwa katika makumbusho hiyo ambapo wakazi wa wilaya za Karatu, Ngorongoro, Monduli na Longido watakuwa sehemu ya wanufaika wa mradi huo.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa mradi huo, Afisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia idara ya urithi wa Utamaduni na Jiolojia PCO Dk. Agness Gidna ameeleza kuwa makumbusho hiyo itakapokamilika itakuwa maelezo ya vituvio mbalimbali ikiwemo Urithi wa Jiolojia unaopatikana katika eneo la Ngorongoro, taarifa zilizohusu milima na mabonde/Kreta za Ngorongoro zilivyotokea, wanyama waliopo, mioto ya asili, mito na maji na umuhimu wake kwa jamii zinazozunguka Ngorongoro.
Vivutio vingine vitakavyokuwepo katika makumbusho ni urithi wa malikale unapatikana Ngorongoro, utamaduni wa jamii za wawindaji, na ukumbi wa maonesho unaobeba zaidi ya watu 100 kwa ajili kuona Ngorongoro live.
Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Jenerali Venance Mabeyo (Mst) ameainisha kuwa bodi ya NCAA pamoja na Menejimenti zinashirikiana na Mkandarasi wa makumbusho hiyo kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vya Kimataifa, kuzingatia ubora na kuhakikisha kufikia mwezi Mei, 2025 jengo hilo liwe limekamilika na watalii kuanza kupata huduma kupitia vivutio vitakavyokuwepo katika Makumbusho hiyo.
Katibu Mtendaji wa UNESCO Tanzania Prof. Hamis Malebo amebainisha kuwa hifadhi ya miamba ya Ngorongoro ndio hifadhi kubwa na yenye maajabu makubwa Afrika kutokana na uwepo wa kreta mbili za ajabu na volcano hai, ambapo Tanzania ni ya pili barani Afrika kuwa na hadhi ya Jiopaki inayotambuliwa na UNESCO ikitanguliwa na Morocco.
ZINAZOFANANA
Orodha ya majeruhi wa jengo la Kariakoo
Rais Samia atoa maagizo kufuatia ajali ya ghorofa la K’koo
Waziri Kijaji afanya mazungumzo na wadau wa COP29