November 14, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wahariri wamparura Waziri Silaa kwa kuwakacha

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa

 

JUKWAA la Wahariri nchini (TEF), limemtahadharisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa kuacha tabia ya kutoshirikiana na taasisi za habari zinazomualika kwenye matukio yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

TEF wamesema kama hatabadili tabia hiyo wanaweza kutoa azimio la kutofanya kazi kama walivyofanya siku za nyuma kwa Ramadhani Omar Mapuri aliyekuwa akiongoza wizara hiyo.

Hayo yamesemwa leo tarehe 7 Novemba 2024, na Deodatus Balile Mwenyekiti wa Jukwaa hilo kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka jijini Dar es Salaam ambapo TEF ilimualika Waziri Silaa kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano huo lakini hakuhudhuria kwenye mkutano huo badala yake akawakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholaus Mkapa.

Balile ameweka wazi kuwa mwenendo wa tabia ya Waziri Silaa kwa wanahabari haufurahishi kwa kuwa hahudhurii shughuli anazoalikwa.

“Hatusemi tunaungana na mtangulizi wale Nape Nnauye kwa aliyoyasema kule Bukoba lakini kwenye Habari alikuwa tukimuita hata usiku wa manene alikuja kuungana na sisi sasa kidogo imekuwa shida kwa Waziri wetu huyu (Silaa) na sisi hatuna mambo ya kusema chinichini maana sisi tukisema chinichini wengine watafanyaje?”

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri

“Amealikwa kwenye mkutano wa wadau wa habari kule Arusha PRST hakwenda, amealikwa kwenye Tuzo za waandishi wa habari (Ejat) hakwenda nikasikia amealikwa Mbeya pia hakwenda, sisi tukasema basi tumpe nafasi akutane na sisi tumualike sisi hakuja anasema Spika amemzuia .”

Balile amesema kuwa kitendo hicho kinawakatisha tamaa wahariri na wadau wa vyombo vya habari kwa kuwa yeye ndio mlezi wa tasnia hiyo.

“Basi sisi tukawaza tukasema Mchungaji mwema huwafahamu kondoo wake na kondoo huijua sauti yake sisi tunaamini kwamba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Kondoo wake ni vyombo vya habari kama kwenye familia anapaswa kukaa nao mezani wakala chakula pamoja wakajadiliana na akaona ni mtoto yupi anakomba mboga na mtoto yupi ni mtiifu ”

Amesema tabia ya waziri Silaa haina afya njema katika tasnia ya habari na wadau wanaojihusisha nayo.

“Mwenendo wa waziri Silaa hautufurahishi na hatutaki kugawana mbao katikati ya bahari wala hatusemi kama anatujaribu lakini akitaka twende katika huo mkondo sisi tupo tayari, anaweza kumuuliza Mzee Mapuli mwaka 2003 alipata kuwa na mvutano na vyombo vya habari na alishuhudia kilichomkuta sasa hatusemi kwamba tunataka kwenda huko lakini tunaomba azipate salamu hizi na ajue kabisa kwamba moja ya majimbo yake ni vyombo vya habari wala hatusemi kwa ukali tunasema ukweli tu.” amesema.

Awali Mkuu wa Edward Mbongolo, alisema waandishi wa habari ni watu muhimu hivyo wachukue hatua za kuhamasisha amani nchini.

About The Author