November 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wahariri uso uso na Waziri Silaa kesho

 

JUKWAA la Wahariri nchini (TEF), linatarajia kufanya mkutano wake mkuu wa nane utakaoanza kesho tarehe 7 na kutamatishwa tarehe 9 Novemba jijini Dar es Salaaam huku mgeni rasmi akiwa Jerry Silaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Anaripoti Faki Sosi Ubwa, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa Habari leo tarehe 6 Novemba 2024 jijini Dar es Salaam, Deodatus Balile ,Mwenyekiti wa TEF, amesema katika mkutano wanachama 130 kati ya 167 wamethibitisha kushiriki huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Weledi wa kitaaluma kwa uhimilivu wa vyombo vya Habari’.

“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Waziri Silaa kukutana na watu wa vyombo vya Habari tangu alipoteuliwa nafasi hiyo. Pia kwenye mkutano huu atakuwepo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

“Pia katika mkutano huo tutajadili na kuingiza wanachama wapya 25, maombi ni mengi tunachambua vigezo vya uzoefu na kiwango cha elimu ambacho ni Shahada ya kwanza na awe amefanya kazi kuanzia miaka 10,” amesema Balile.

Amefafanua kuwa, kutakuwa na mada kuu mbili, ikiwemo kuhusu utendaji wa vyombo vya Habari na uchumi wa vyombo vya Habari.

“Tutaangalia katika mwaka huu mzima tangu umeanza ni mambo gani yametokea kwenye taaluma yetu, tumefanya jambo gani ambalo ni zuri kama waandishi wa Habari, tumepatia wapi na tumekosea wapi. Kwa maana tusipojitathimini hatuwezi kujua kama tunakwenda vizuri au hatuendi vizuri.

“Mada ya pili tutaangalia uchumi wa vyombo vya Habari, tunajua mwaka huu Juni iliwasilishwa taarifa ya hali ya vyombo vya habari mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa hiyo tunakwenda kuangalia vyombo vyetu vina hali gani kwasasa, tufanye nini kuimarika zaidi na jambo zuri ambalo tumesema tuanze nalo wahariri ni tuache kulialia,” amesema na kuongeza:

“Hatutabadilisha hali zetu kwa kila siku kulia hadharani, tufanye kazi kubadili hiyo hali mbaya kuwa hali nzuri, tunavyo vyombo vya Habari ambavyo vinafanya vizuri na kulipa watu wake vizuri, kulipa bima kwahiyo tutabadilishana ujuzi.

About The Author