November 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mpina rasmi bungeni kesho

Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina

 

MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, anamaliza adhabu yake ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge, aliyopewa tarehe 24 Juni, mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Aliadhibiwa kwa kosa la kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge, huku akizuiwa kufika kwenye maeneo ya Bunge, wala kujihusisha na shughuli zozote za Bunge.

Baada ya kuadhibiwa, Mpina hakuhudhuria vikao vitano vya Bunge la Bajeti mwezi Juni, Bunge la Septemba ambalo lilikuwa na vikao tisa na kimoja cha jana.

Azimio la Bunge kumsimamisha mbunge huyo, lilifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Ally Makoa, kulieleza Bunge kwamba, Mpina alitiwa hatiani kwa kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge.

Uamuzi wa kumfungia Mpina kuhudhuria vikao 15, ulifikiwa baada ya wabunge wengi kupiga kura ya kuitikia ndio.

Baada ya wabunge kuchangia, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliwauliza wanataka Mpina afungiwe kwa vikao 10 kama lilivyokuwa pendekezo la Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, walitikia wachache na alipouliza wanaotaka afungiwe vikao 15, waliitika wengi.

Awali, Mpina alipaswa kuthibitisha ukweli kama Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alikuwa amelidanganya Bunge kama alivyomtuhumu awali.

Ilidaiwa kwamba, Mpina hakuthibitisha madai hayo ndani ya Bunge na badala yake, aliwasilisha Ushahidi kwa Spika na kisha kuitisha mkutano na waandishi wa habari, kueleza kile alichokuwa amekipeleka kwenye ofisi ya spika kama Ushahidi.

Kitendo hichi ndicho kilichomfanya spika ampeleke kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliyopendekeza asimamishwe kuhudhuria vikao 10.

About The Author