October 30, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kigahe: Rahisisheni zaidi mazingira ya urasimishaji biashara

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe

 

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amehimiza urasimishaji wa biashara, huku akiuelekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), kurahisisha taratibu za usajili. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).

Kigahe ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa pili wa Brela na wadau uliowakutanisha wafanyabiashara wadogo na wakubwa, sekta ya umma na binafsi.

Ametoa maelekezo hayo wakati ambao mfumo wa wakala huo, unasomana na taasisi 12 ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na benki mbalimbali.

Amesema mazingira rahisi na rafiki ya urasimishaji, yatawapa wafanyabiashara wigo wa kukua na kukuza uchumi wa nchi, kwa kuwa watatambulika na mamlaka mbalimbali.

Amesema nyenzo muhimu ya kurahisisha usajili, ni mifumo ya kitaasisi kusomana kwa lengo la kutoa huduma zote kwa njia ya mifumo, ili kuondoa usumbufu na kero, kwa wananchi kulazimika kuwa na nyaraka ambazo zikiwekwa kwenye mfumo mmoja, zinapaswa kusomwa kwenye taasisi nyingine ya serikali.

“Utendaji na ufanisi wa Brela ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu, kwa sababu hapa ndipo biashara zinapozaliwa na kuanzishwa. Tuweke mazingira bora ya kurasimisha biashara zote,” amesema.

Kigahe ameongeza: “Na wenzetu wa Halmashauri mtusaidie, tungependa kuona biashara zote ndogo, za kati na kubwa zinarasimishwa. Bado tuna biashara nyingi ambazo haziko rasmi.”

Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira bora, wezeshi na shirikishi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, ili kuwa na uchumi endelevu.

Kigahe amepongeza utaratibu wa Brela kukutana na wadau, ambao maoni yao yataiwezesha taasisi hiyo kujitathmini, ili kufanyakazi kwa ufanisi na tija.

“Nitoe rai kwa Taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu huu, kuiga mfano huu mzuri ili kujipima kwa kupata maoni ya wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa, amesema lengo la mkutano huo ni kujadili fursa, mafanikio na faida, ya mifumo ya serikali kusomana, katika kurahisisha huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Amesema Brela inatoa huduma zake kwa njia ya mtandao, jambo lililowezesha kupunguza muda wa kusajili kampuni na biashara, kutoka takribani mwezi mmoja hadi siku moja, gharama na kero, kwa wafanyabiashara ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

“Hii ni hatua kubwa katika uboreshaji wa mazingira ya biashara. Mfumo wa usajili mtandaoni umetimiza miaka sita sasa, ni dhairi teknolojia na baadhi ya sheria zimebadilika sana…tumeanza maboresho ya kuufanya uwe bora na rafiki zaidi,” amesema Nyaisa.

Ameongeza kuwa: “Maboresho haya yamezingatia uwepo wa huduma zingine, mfano upande wa leseni za biashara, Brela inaendelea na mashauriano na mamlaka zingine ili kutumia mfumo mmoja wa leseni za biashara, utakaotoa leseni za kundi A (viwanda na kampuni kubwa), zinazotolewa na Brela na zile za kundi B zinazotolewa na Halmshauri.”

“Uanzishwaji wa mfumo huu mmoja wa leseni utaisaidia kuipa serikali takwimu sahihi pamoja na kuthibiti upotevu wa mapato kwa kuondoa leseni za kuandikwa kwa mikono,” amefafanua Nyaisa.

Nyaisa amesema wakala huo umeanza kuratibu maoni ya kuandika sera ya taifa ya Miliki Ubunifu, inayoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kushirikiana na wadau.

Mkutano huo umehudhuriwa na taasisi za umma na binafsi, wawekezaji, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wajasiriamali, wabunifu na mawakili.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini.’

About The Author