October 30, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wazalishaji mbegu feki wadakwa Magu, DC Nassari atoa ujumbe kwa wakulima

 

VIJANA wawili wamekamatwa na vyombo za ulinzi na usalama wilayani Magu mkoani Mwanza kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza mbegu feki za mahindi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 41 pamoja na dawa feki za mifugo hali inayotajwa kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuwainua wakulima na wafugaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Magu, Mwanza …  (endelea).

Vijana hao Mahe James Raymond (28) na Omary James Mahe (27) wamekamatwa juzi Jumatano tarehe 23 Oktoba, 2024 na jeshi la polisi wilayani Magu kwa kushirikana na maofisa ukaguzi wa wilaya ya Magu baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa katika kituo cha polisi wilaya ya Magu, walikuwa wakiendesha shughuli zao za uzalishaji wa mbegu feki katika moja ya nyumba iliyopo mtaa wa Isandula Juu, kata ya Kandawe – Magu Mjini.

Akizungumza na waandishi wa Habari jana tarehe 24 Oktoba, 2024 baada ya kukagua mbegu hizo feki za mahindi pamoja na dawa feki za mifugo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari amesema baada ya kupekua nyumba hiyo wamebaini zaidi ya magunia 20 ya mahindi ambayo yalikuwa yanaandaliwa kuwekwa rangi kabla ya kupakiwa kwenye vifungashio.

Amesema maofisa hao wa halmashauri ya wamekamata mbegu feki za mahindi tani 2.6 (kilo 2,600) zikiwa kwenye vifungashio vya kampuni ya DK zenye namba tofauti tofauti.

“Mbegu hizo zinaonekana ni mbegu kutoka Kenya lakini kwa uchunguzi wetu tumegundua ni mahindi yanayonunuliwa kwenye masoko yetu yanaletwa hapa yanapakwa rangi nyekundu (PVA) na baada ya kulowanishwa kwenye maji yanaanikwa, yakishakauka yanafungwa kwenye vifungashio vya kisasa kabisa. Kwa mkulima wa kawaida hawezi kujua kirahisi kuwa hizi mbegu feki kwani zipo pamoja na stika zake.

“Tumewasiliana na wenzetu wa TOSC ambao ndio mamlaka inayohusika na mbegu wamefanya uchunguzi na kubaini kweli ni feki. Lakini pia kwa habari tulizozipata jana (juzi) ni kwamba kuna mzigo mwingine ulitoka kuingia mikoa jirani kwa maana nyingine ni kuwa mkulima wa nchi hii hatendewi haki wakati serikali inahangaika kuinua kilimo.

“Rais Samia Suluhu Hassan inahangaika kufufua miradi mbalimbali ya umwagiliaj, wizara ya kilimo inahangaika na program mbalimbali ikiwamo BBT na nyingine, lakini kuna watu wanarudisha nyuma jitihada hizo kwa kumuuzia mkulima mbegu feki.

“Mfano mamlaka ya hali ya hewa (TMA) imesema mvua za vuli msimu huu zitakuwa za wastani na chini ya wastani, hivyo tulikuwa tunamshauri mkulima kulima mahindi kwa kutumia mbegu ambazo ni za muda mfupi lakini unaweza kumwambia mkulima anunue DK 777 za muda mfupi kumbe mbegu yenyewe ni feki hili ni kosa kubwa linarudisha nyuma jitihada za serikali kumkwamua mkulima,” amesema.

Amesema wilaya ya Magu kwa kushirikiana na TOSC, wamekagua mizigo ya watuhumiwa hao ndani ya nyumba hiyo na kubaini dawa nyingi za mifugo ambazo zinaonekana zimeingizwa kutoka nchi jirani lakini hakuna nyaraka za uingizaji, kodi iliyolipwa, nyaraka zinazoonesha bidhaa ni halali au labda inafaa kwa matumizi kwamba ni sumu au si sumu.

“Nitoe rai kwa watanzania na hususani wakulima, wakati serikali inaendelea kuchunguza jambo hili kwa kuangalia ni kiasi gani cha mbegu kimeenda kwenye maduka au masoko yetu ni vema wakulima wakawa makini ili wasiwe wahanga wa kuuziwa mbegu feki ambazo zimefungwa kwenye vifungashio vinavyoonekana kama vile halali.

“Wakumbuke kuangalia kama kuna stika ya TOSC au stika inayoonesha ubora wa mbegu kutoka nje, pia wale wafugaji ambao wanatumia dawa za mifugo ya ng’ombe, kondoo, mbuzi, nguruwe wa kila aina tumeona pale kwa hiyo watalaam wataendelea kufanyia kazi kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa,” amesema.

Naye Mkaguzi wa mbegu na Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kanda ya Ziwa, Ayoub Mushema amesema mbegu hizo ni feki kwa sababu hazina lebo ya udhibiti wa ubora ya TOSC wala ile ya mbegu zinazotoka nje.

“Tunashukuru uongozi wa wilaya na polisi kuwa walipopata taarifa walichukua hatua za haraka. Wapo watu wanaohujumu kwani kitendo cha kumuuzia mkulima mbegu feki ni hasara, tunatoa wito waendelee kushirikiana na polisi na sisi watdhibiti ubora wa mbegu,” amesema.

Aidha, Afisa Mfugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Dominic Mwakapemba ametoa wito kwa kuhakikia kwa makini vifungashio kama vina taarifa za mzalishaji, lebo mdhibiti ubora na pia kuchukua risiti kuitunza.

About The Author