TANZANIA na Pakistan, zimekubaliana kupanua wigo wa ushirikiano ili kukuza uhusiano wa nchi hizo mbili, wakizingatia vipaumbele na manufaa ya wananchi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wakizungumza pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Muhammad Ishaq Dar, wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika kilimo, teknolojia, viwanda vya nguo na biashara.
Waziri Kombo ameishukuru Pakistan, kwa ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania kwa takribani miaka 60 sasa.
Amepatia Dar kitabu picha (Photographic Journey: 60 Years of the United Republic of Tanzania), kinachoonesha historia ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika picha, ambacho dibaji yake, imeandikwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola wamekutana leo Oktoba 24, 2024 kujadili na kupitisha ajenda Kuu ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), ya Ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ya kimaendeleo (One Resilient Common Future).
Mkutano huo umeridhia agenda za ustahimilivu wa mazingira, ustahimilivu wa uchumi, ustahimilivu wa watu katika jamii na ustahimilivu wa taasisi zinazolinda demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu kuwekwa mezani kwenye mkutano wa ngazi za juu.
Mbali na Agenda hizo, Mawaziri pia wamepokea na kupitisha taarifa za Jukwaa la Wanawake, Jukwaa la Biashara, na Jukwaa la Vijana yaliyokuwa yakiendelea kwa wiki hii.
Waziri Kombo ameshiriki Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya, Fiamē Naomi Mataʻafa, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Samoa.
Vipaumbele vya Tanzania katika Mkutano wa CHOGM ni pamoja na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kuwezesha vijana na wanawake kiuchumi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kwa nchi wanachama.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia kesho Oktoba 25 na 26, 2024, ambapo Waziri Kombo atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo unafanyika jijini Apia, Samoa.
ZINAZOFANANA
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya
Upelelezi wakwamisha kesi ya Boni Yai