November 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waziri Mkenda aipa kongole NBC utoaji Elimu ya Fedha kwa wananchi

 

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Benki ya NBC kwa jitihada na mkakati wake wa kutoa elimu kuhusu matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanafunzi na wananchi hususani wa maeneo ya vijijini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda mbali na kuchochea kasi ya ukuaji uchumi jumuishi, jitihada za benki hiyo zinaunga mkono utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Serikali wa Maendeleo ya Sekta ya fedha hasa utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

Waziri Mkenda aliyasema hayo mapema leo alipotembelea banda la Benki ya NBC lililopo kwenye maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha ambayo kitaifa yanafanyika kwenye viwanja vya CCM Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Alisema benki hiyo ni miongoni mwa benki ambazo zinatoa huduma nzuri kwa wananchi wakiwemo wa maeneo ya vijijini ambako taasisi nyingi za fedha hazijafikisha huduma hizo.

“Binafsi ni mteja wa benki ya NBC hivyo ni mmoja wa mashuhuda muhumu kwenye jitihada hizi za NBC. Mmekuwa mkiwafikia wananchi hadi vijijini kabisa mkitoa elimu na huduma zenu. Nawaomba muendelee hivyo hivyo, lengo la serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wote wawe wanatumia mifumo rasmi ya kifedha ifikapo 2026,” alisema Prof. Mkenda.

Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Mwanjelwa, Khalid Omary alisema benki hiyo inaendelea kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo wa kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi hasa wa maeneo ya vijijini kwa kuanzisha huduma mbambali mahususi kwa makundi hayo.

Alisema pamoja na uwekezaji mkubwa kwenye utoaji wa huduma za kibenki kwa njia za kidigitali, benki hiyo imeendelea kuwafikia wananchi kwa kufungua matawi mapya ya benki, kuweka mashine za kutolea fedha (ATM) na kuwatumia mawakala wa huduma za kifedha walioko katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijijini.

 

“Uwepo wetu kwenye matukio kama haya umekuwa ukihusisha zaidi utoaji wa elimu za kifedha kwa wananchi wa aina mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo pamoja na wananchi wa makundi yote ya kiuchumi wanaotembelea mabanda yetu ya maonyesho.’’

“Kupitia jitihada hizi tumefanikiwa kubadili kwa kiasi kikubwa mitazamo ya wananchi kuhusu matumizi ya taasisi hizi rasmi za kifedha na wengi wameweza kufungua akaunti na wamekiri kuachana na njia za kizamani na hatarishi za kuhifadhi fedha zao ikiwemo kutunza kiasi kikubwa cha fedha ndani ya nyumba zao,’’ alisema Omary.

Alisema kufuatia mwamko huo. Kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi kunufaika na huduma mbalimbali za kifedha kupitia benki hiyo ikiwemo huduma ya mikopo hususani ya biashara na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa biashara zao.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Huduma za Fedha kitaifa yanafanyika kwa mara ya nne nchini ambapo kwa mkoa wa Mbeya yanafanyika ni kwa mara ya kwanza.

About The Author