October 17, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Gachagua akalia kuti kavu, adaiwa kukimbizwa hospitali

 

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ameshindwa kujitetea mbele ya Bunge la Seneti, baada ya kudaiwa kuugua na kupelekwa hospitali. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Wakili wake, Paul Muite, ameliambia Bunge la Seneti kwamba Gachagua ni mgonjwa na kuwa yuko hospitalini, saa chache kabla hajajitetea mbele ya maseneta.

Gachagua alitakiwa kujitetea mbele ya Bunge la Seneti leo mchana na alipotakiwa kuingia kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili, hakuwepo.

Baada ya kutoa taarifa ya kuwa Gachagua ni mgonjwa, Spika wa Bunge la Seneti, Amason Kingi, aliomba maoni ya wajumbe ambao wameoamua kuahirisha kupiga kura hadi jioni ili kufuatilia hali ya afya ya kiongozi huyo.

Spika Kingi ameahirisha kikao hadi saa 11:00 jioni ya leo tarehe 17 Oktoba 2024.

Bunge la Seneti lilianza kumjadili Gachagua jana ikiwa ni hatua ya mwisho ya kumuondoa madarakani, baada ya Bunge la Kitaifa kumpigia kura Jumanne ya wiki iliyopita.

Naibu Rais huyo anakabiliwa na mashtaka 11 yakiwamo ufisadi, kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu serikali, ambayo hata hivyo ameyakanusha.

Ili kukamilisha azma ya kumtimua kwenye wadhifa huo, theluthi mbili ya wajumbe 67 wa Seneti inapaswa kupiga kura kuunga mkono azimio hilo. Baada ya kusikiliza pande zote, Seneti litatoa uamuzi wa mwisho ndani ya siku 10.

Iwapo ataondolewa madarakani, Gachagua hatoruhusiwa kushika wadhifa wa umma nchini humo.

Mjadala wa leo unatokana na kile kilichoamuliwa na wabunge kupitia kura ya kumwondoa kwenye wadhifa huo Jumanne ya wiki iliyopita.

Gachagua alitimuliwa na bunge Jumanne tarehe 08 Oktoba 2024, baada ya wabunge 281, kupiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwake ofisini.

Katika kura za wiki iliyopita, wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo, na 44 waliipinga; na kufikia theluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa ofisini.

Mjadala wa Seneti unaendelea baada ya Mahakama Kuu ya Kenya, kutupilia mbali ombi la mwanasiasa huyo, aliyetaka mhimili huo uzuie kujadiliwa kwake na Bunge la Seneti, akidai kuwa hoja ya kumtimua ilitokana na madai ya uongo yaliyochochewa kisiasa.

Mahakama imetupa hoja ya Gachagua, ikieleza kuwa ni mchakato wa kikatiba ambao hauwezi kuingiliwa na mhimili mwingine.

Leo, Naibu Jaji Mkuu wa Kenya, Philomena Mwilu, amesema iwapo mchakato wa kumtimua Naibu Rais Gachagua utarejea tena mahakamani, majaji watafuata utaratibu ulioainishwa kwenye katiba.

About The Author