ILANI ya asasi za kiraia (AZAKI), imetaja sifa 10 za kiongozi anayeweza kuisaidia nchi kimaendeleo, ikiwamo anayesimamia na kuheshimu Katiba, kulinda haki za binadamu na kuliunganisha taifa. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, ameiambia MwanaHALISI kuwa sifa hiyo kubwa ndiyo inayotajwa na wananchi kwenye ilani ya AZAKI ambayo wameisambaza kwenye vyama vya siasa.
Katika ilani hii tumeeleza ni kiongozi yupi anaweza kutupeleka katika Tanzania tuitakayo
“Asasi za Kiraia (AZAKI), kwa umoja wetu tunakumbusha kuwa kiongozi anayefaa kuiongoza Tanzania tuitakayo ni mtetezi na mlinzi wa katiba na haki za binadamu. Hii ni sifa kuu kwa kiongozi yeyote yule kuanzia ngazi za chini za serikali mpaka ngazi za juu,” amesema.
Amesema kiongozi wa kuchaguliwa na wananchi kuanzia serikali ya Mtaa au Kitongoji, anapaswa kuwa na maono ya kulileta Taifa pamoja, kujenga Tanzania upya, kueneza mshikamano na kuhamasisha umoja wa kitaifa utakaojengwa kwa misingi ya kikatiba.
“Awe na utashi na busara za kiuongozi na asiyekubali kupitisha na kusimamia sheria mbovu, zenye kukandamiza utawala bora, demokrasia na haki za binadamu,” amefafanua.
Amesema kiongozi pia anapaswa kuwa muwazi katika utendaji kazi wa serikali na anayethamini ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya umma kwa maendeleo ya Taifa.
Ole Ngurumwa ametaja sifa nyingine kuwa ni kiongozi anapaswa kuwa muumini wa maendeleo shirikishi, muwajibikaji na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi yenye tija kwa umma ikiwamo kuwajibisha viongozi wazembe, bila kuvunja sheria za nchi.
“Kiongozi lazima awe mwadilifu, asiyetoa wala kupokea rushwa, mzalendo kwa nchi yake na aliye tayari kuondoa mifumo ya rushwa na ubadhirifu nchini. Mahiri katika kusimamia na kulinda rasilimali za nchi ikiwemo kupinga mikataba ambayo haina tija na anayeamini katika misingi ya usawa wa kijinsia, ushiriki na ujumuishi,” amesema.
ZINAZOFANANA
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya
Upelelezi wakwamisha kesi ya Boni Yai