WADAU wa kilimo ikolojia hai kutoka taasisi 16 nchini wanatarajia kushiriki katika maonesho ya kitaifa ya nanenane 2024 ambayo yaanza tarehe 1 hadi 8 Agosti mwaka huu mkoani Dodoma. Anaripoti Matilda Peter, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kikosi Kazi cha Mbegu Asili nchini, Abdallah Mkindi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jana Jumatatu jijini Dar es Salaam.
Mkindi amesema wanashiriki maonesho ya mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kilimo hai ambao umezinduliwa hivi karibuni na serikali.
Ametaja taasisi za kilimo ikolojia hai ambazo zinashiriki nanenane 2024, ni Mtandao Baionuai Tanzania (TABIO), Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Biovision Africa Trust (BVAT), SwissAid Tanzania, Floresta, na Shirikisho la Vyama vya Wakulima Wadogo Tanzania (SHIWAKUTA).
Nyingine ni Agroecology Hub-SUA, Kijani Hai, IDP, We Effect, VI Agroforestry, Farm Radio International, Taasisi ya Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Safari Organic Co Ltd na MC Donald Organic Products.
“Mwaka huu tumeandaa mabanda yasiyopungua sita ambayo yataonesha teknolojia na bidhaa mbalimbali, mbegu za asili, pembejeo za kilimo kama mbolea na dawa za kuuwa wadudu wasumbufu,” amesema Mkindi.
Mratibu huyo amesema wao kama wadau wakuja pamoja kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa na kuleta mabadiliko kwenye sekta ya kilimo hasa kilimo ikolojia hai.
Mkindi ambaye pia ni Mratibu wa TABIO, amesema katika maonesho hayo watakuwa na wakulima zaidi ya 20 ambao wanazalisha mazao mbalimbali kama mahindi, maharage, mpunga, viazi na mengine kwa njia ya asili.
Amesema pia kupitia maonesho hayo watakuwa na kauli mbiu ya mbegu ni uhai hali ambayo itasaidia watunga sera na wananchi kutambua faida ya mbegu za asili kwa watumiaji na nchi.
Mratibu huyo amesema katika kuhakikisha dhana ya mbegu ni uhai inafikia jamii kubwa wameandaa mabango na midahalo kwa wadau wa sekta ya kilimo hasa kilimo ikolojia.
“Hizi siku nane za maonesho ya nanenane tumejipanga kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu faida za kutumia vyakula ambavyo vimetokana na mbegu asili, lakini pia tutaonesha bidhaa zote ambazo zina faida katika kilimo,” amesema.
Mkindi amesema faida ya mbegu asili ni urithi wetu, zina virutubisho, wakulima wanazimiliki, zinatunza na kulinda baionuai, zina ustahimilivu na mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwa ujumla.
Mratibu huyo amesisitiza kuwa iwapo wakulima watajikita katika kilimo ikolojia hai watahakikishia jamii usalama wa chakula na afya kwa watumiaji.
ZINAZOFANANA
Serikali: Sera ya Bima ipo hatua za mwisho kukamilika
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya