HUKUMU ya kesi ya jinai ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mmoja mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es saalam (jina limehifadhiwa), inatarajiwa kutolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kesi hiyo Namba 23476 ya Mwaka 2024, inawakabili washtakiwa wanne, wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105, Clinton Damas, askari magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson na Amin Lema.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani tarehe 19 Agosti 2024 na kusomewa mashtaka hayo mawili waliyodaiwa kumtendea binti anayetambulika mahakamani kwa jila la XY.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa iliyopita, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando, alisema kila kitu kilichotakiwa kwenye kesi hiyo kimekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni uamuzi wa mahakama.
Alisema mwishoni mwa wiki iliyopita, walifanya mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo wa kesi hiyo na kwamba wamewasilisha hoja kuhusu kasoro zilizojitokeza wakati wa usikilizaji.
“Tumepata nafasi ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho, kuhusu mwenendo wote wa kesi kuanzia hati ya mashtaka, ukamataji, utambuzi, mashahidi, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kwa muda wa saa tatu na upande wa serikali nao umewasilisha yao… kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa mahakama,” alisema Ngamando.
Alisema mwenendo wa kesi ulikuwa mzuri na kumbukumbu zilichukuliwa vizuri.
Naye wakili Godfrey Wasonga, ambaye yuko upande wa utetezi, alisema wapo tayari kwa uamuzi utakaotolewa na mahakama.
Utetezi wa washtakiwa hao ulifungwa Alhamisi tarehe 26 Septemba 2024, kwa watuhumiwa kujitetea bila kuwa na kielelezo chochote.
Awali, upande wa utetezi ulisema ungekuwa na mashahidi 10 na vielelezo sita. Katika kesi hiyo maarufu ‘waliotumwa na afande’ iliyosikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma; kwa upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 18 na vielelezo 12 kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule, washtakiwa hao baada ya kusomewa mashataka walikana na kutokana na unyeti wa kesi hiyo, ilisikilizwa faragha na watuhumiwa walinyimwa dhamana.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe