RAIS Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa wakulima, akiielekeza Wizara ya Kilimo, kuanzia msimu ujao wa mavuno, kuwalipa wakulima moja kwa moja na vyama vikuu vya ushirika badala ya utaratibu wa sasa wa kupitishia malipo hayo kwenye Vyama vya Msingi (AMCOS).
Amesema utaratibu wa kupitisha malipo AMCOS, unawacheleweshea wakulima malipo yao na kuongeza makato.
Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara yake mkoani Ruvuma, uliofanyika katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Amesema serikali itaendelea na utaratibu wa Stakabadhi Ghalani, Soko la Bidhaa (TMX) na minada kwa njia ya mtandao, ili kunufaisha mkulima moja kwa moja na kupata takwimu sahihi za kilimo nchini na kuiwezesha Tanzania isomeke katika ramani ya biashara ya kilimo na kuweka urari mzuri kwenye biashara ya kimataifa.
Pia, amesema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), itaendelea kuimarishwa ili iendelee kuwa soko la uhakika la mazao ya nafaka na kulihakikishia taifa usalama wa chakula.
ZINAZOFANANA
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya
Upelelezi wakwamisha kesi ya Boni Yai