WhatsApp Image 2026-04-13 at 3.22.27 PM

 

MWENYEKITI wa Chama cha ACT – Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman akiambatana na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Juma Duni Haji (Babu Duni), leo 13 Aprili 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera pamoja na ujumbe wake Mjini Zanzibar .Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).

Kikao hicho kilitoa fursa kwa pande hizo kujadili kwa kina hali ya kisiasa nchini, hususan mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kuanzia maandalizi yake, mwenendo wa siku za upigaji kura Oktoba 28 na 29, hadi matokeo na athari zilizojitokeza baada ya uchaguzi huo.

Mazungumzo hayo yalilenga pia kuangazia changamoto zilizojitokeza na namna zinavyoendelea kuathiri utulivu wa kisiasa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Othman Masoud Othman aliwasilisha rasmi ripoti ya chama hicho kuhusu uchaguzi huo iliyopewa jina la “Uchaguzi Uliovurugwa”, akieleza kuwa ripoti hiyo inaelezea kwa kina kasoro zilizojitokeza pamoja na mapendekezo ya hatua za haraka na za muda mrefu ili kurejesha imani ya wananchi katika mifumo ya uchaguzi.

Alisisitiza kuwa ACT Wazalendo inaamini katika suluhu ya kudumu itakayojengwa juu ya misingi ya haki, uwazi na utawala bora.

Aidha, alibainisha kuwa chama hicho tayari kimechukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria kutafuta haki na kuleta maridhiano, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mazungumzo ya kitaifa yatakayowahusisha wadau wote wa siasa ili kuondoa mivutano inayojirudia kila baada ya uchaguzi Zanzibar.

Kwa upande wake, Lazarus Chakwera alisisitiza umuhimu wa pande zote zinazohusika kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kushirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya hali ya kisiasa iliyopo.

Akieleza kuwa Jumuiya ya Madola iko tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhimiza mazungumzo yenye tija na yanayolenga kuimarisha demokrasia.

Kikao hicho kinatajwa kuwa sehemu ya jitihada pana za kimataifa za kufuatilia na kusaidia mchakato wa kidemokrasia nchini, huku kikitarajiwa kufungua milango ya mazungumzo mapya yatakayosaidia kupunguza mvutano wa kisiasa na kujenga mustakabali imara wa kisiasa Zanzibar.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!