April 9, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwaka mmoja wa Lissu gerezani

Tundu Lissu akiwa mahakamani

Spread the love

 

NI mwaka mmoja umepita, tangu kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania (Chadema), Tundu Lissu, kukamatwa na kushikiliwa gerezani kwa tuhuma za uchochezi na uhaini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu alikamatwa tarehe 9 Aprili 2026, huko Mbinga, mkoani Ruvuma, katikati ya kampeni ya kuhamasisha msimamo wa chama chake wa “No Reforms, No Election” – Bila Mabailiko, Hakuna Uchaguzi.

Alifikishwa Mahakama ya Kisutu, tarehe 10 Aprili 2025 na kupelekwa moja kwa moja Gereza Kuu la Keko, jijini Dar es Salaam na kuhamishiwa Ukonga anakozuiliwa mpaka sasa.

Mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, ametimiza mwaka mmoja tangu kukamatwa na kuwekwa gerezani, huku kesi yake ikegeuka kuwa kivutio kimataifa, ikichochea mjadala kuhusu haki za kikatiba, uwazi wa mahakama na uhuru wa kisiasa nchini mwake.

Kesi dhidi ya Lissu, ni mojawapo ya kesi kubwa zaidi za kisiasa nchini Tanzania tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Wafuasi wake wanadai kuwa kesi dhidi ya kiongozi wao, imesheheni msukumo wa kisiasa, lakini serikali ikijitetea kuwa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria za nchi inayolenga kulinda usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi, Lissu amekamatwa kutokana na hotuba zake kuhamasisha umma kupinga kufanyika kwa uchaguzi, jambo ambalo serikali ilisema linakiuka sheria za uhaini na usalama wa taifa.

Hata hivyo, Lissu anasema, hakuna sheria yoyote nchini inayokataza watu kupinga uchaguzi au kuzuia uchaguzi. Anasema, uchaguzi wa Tanzania umekuwa ukivurugwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, kwa maslahi binafsi.

Anatolea mifano ya chaguzi nne zilizopita – uchaguzi mkuu wa 2020 na 2025, pamoja na uchaguzi wa serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na 2024.

Lissu aliyeingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama chake, uliofanyika tarehe 21 Januari mwaka jana, ameonekana kuwa tishio kwa walioko madarakani, kutokana na misimamo yake isiyoyumba ya kupigania rasimali za umma, demokrasia na uhuru wa kujielekeza.

Katika uchaguzi huo, Lissu alimshinda Freeman Mbowe, ambaye alionekana kuwa kipenzi cha serikali iliyopo madarakani, hususani uongozi wa sasa wa Rais Samia Suluhu Hassan, hadi baadhi ya wafuasi wa Chadema, kudiriki kumtuhumu mwanasiasa huyo, “kulambishwa asali na watawala.”

Kwa sasa kesi ya uhaini inayomkabili Lissu imehamia Mahakama ya Rufani, baada ya serikali kuiomba mahakama hiyo, kufanyia mapitio uamuzi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo Dar es Salaam, uliotupilia mbali notisi yake ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.

Lissu aliiambia Mahakama kuwa Kifungu cha 8(2D) cha sheria ya Mamlaka ya Rufaa, hakiruhusu rufaa wala mapitio wala marejeo ya maamuzi ya mahakama ambayo hayamalizi shauri la msingi.

Aksema anafahamu rufaa hiyo imewasilishwa ili aendelee kukaa gerezani. Ingawa upande wa Serikali unasema, ni haki ya kisheria kukata rufaa.

Kinachosubiriwa sasa ni jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa kukaa, kufanya mapitio ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kutoa uamuzi. Mpaka sasa, tarehe rasmi ya usikilizaji wa shauri hilo, bado haijatangazwa.

Hata hivyo, jambo lililowazi ni kwamba kesi ya Lissu, imeibua mwangi mkubwa kwenye mashirika ya kutetea haki za binadamu ulimwenguni.

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Haki za Binadamu, imekuwa ikitaka serikali kumuachia huru mwanasiasa huyo kwa melezo kuwa kushikiliwa kwake, ni kinyume na sheria za kimataifa.

Kamisheni hiyo imesema, serikali uchukue hatua zinazohitajika kurekebisha hali ya Lissu mapema, kwa kufuata kanuni za kimataifa, zilizoainishwa katika tamko la haki za kibinadamu na mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa.

“Lissu anashikiliwa kinyume na sheria za kimataifa. Hivyo mamlaka inapaswa kumuachia huru na kulipa fidia kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” imeeleza taarifa hiyo, iliyotolewa tarehe 13 Februari mwaka huu.

About The Author

error: Content is protected !!