April 6, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chadema wamejitosa sakata la mafuta

John Heche, Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokraisa na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema, kuna kikundi cha watu wachache nchini, kilichojimilikisha uchumi wa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu, tarehe 6 Aprili 2026, Heche alisema, “…kuna ma- caretel (Kundi la wafanyabiashara), ambao wanajimilikisha uchumi wa Tanzania,” akihusisha na kampuni moja kupewa kibali cha kuagiza mafuta na kuyauza kwa bei ya juu.

Alisema, kuna taarifa ya kuwepo kampuni moja yenye ukaribu na watu wakubwa walioko serikalini ndiyo ilipewa tenda na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (PTDC), kuagiza mafuta na yenyewe ndiyo inasimamia kuweka bei za mafuta hayo.

Heche hakutaja jina la kampuni hiyo, lakini MwanaHALISI limedokezwa jina la kampuni hiyo, iliyoanzishwa miaka ya tisini.

“Tunazo taarifa kwamba makampuni moja yenye ubia na watu walioko serikalini, ndio ilipewa tenda pekee yake ya kuagiza mafuta na TPDC. Na yenyewe ndio inadhibiti bila ushindani bei za mafuta na kuwasababishia Watanzania matatizo makubwa,” alieleza.

Serikali ya Tanzania ilitangaza bei mpya ya juu ya mafuta iliyoanza kutekelezwa tarehe 1 Aprili, ambayo imeibua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi, kufuatia nishati hiyo, kupanda kwa kiwango kikubwa.

Kulingana na Mamlaka ya udhibiti ya huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA), kupanda kwa bei hizo kumetokana na ongezeko kubwa linalosababishwa na kinachoitwa, “mzozo unaoendelea mashariki ya kati dhidi ya Iran.”

Bei ya lita ya petroli jijini Dar Es Salaam imepanda kwa shilingi 956 za Tanzania ambayo ni sawa na dola senti 37 na kuzua hisia kali miongoni mwa raia wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa bei mpya mjini Dar es Salaam Petroli sasa itauzwa kwa shilingi za Tanzania 3,820, Dizeli Sh 3,806, Mafuta ya Taa Sh 3,684.

Mjini Tanga petroli itauzwa Sh 3,881, Dizeli Sh 3,867 huku Mafuta ya Taa yakiuzwa kwa Sh 3,745.

Hata hivyo, serikali kupitia TPDC, ilinukuliwa ikisema, inayo akiba kubwa ya mafuta yanayoweza kutosha matumizi yake kwa muda wa miezi mitatu. Lakini mafuta yamepanda ndani ya mwezi mmoja wa mzozo huo.

About The Author

error: Content is protected !!