KAMPUNI ya Taifa Gas nchini Tanzania, imetangaza kwamba haitapandisha bei ya gesi ya majumbani (LPG), licha ya kuongezeka kwa bei ya gesi ulimwenguni kwa 43 asilimia. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam …(endelea).
Taarifa ya kampuni hiyo, imeeleza kuwa hatua hiyo, ni sehemu ya juhudi zake za kuendeleza upatikanaji nafuu wa nishati hiyo, pamoja na kupunguza athari za mabadiliko ya soko la kimataifa kwa wateja wake.
Kampuni ya Taifa Gas inasema, “Soko la kimataifa la gesi ya kupikia, limekumbwa na ongezeko kubwa la bei katika wiki za hivi karibuni na hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za ununuzi katika minyororo ya ugavi na usambazaji duniani.
“Katika mazingira haya ya sasa, tunayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wateja wetu kwa kubeba athari za ongezeko hilo la gharama ya nishati ya kupikia kwa kutokuongeza bei huku tukihakikisha upatikanaji endelevu wa gesi safi na ya kuaminika,” ameeleza Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius.
Taifa Gas imesema, kipaumbele chake kwa sasa ni kuhakikisha bei hiyo ya nishati haiongezeki, huku ikitambua kuwa gesi ya kupikia, ni nishati muhimu katika kaya na biashara ndogo ndogo nchini.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, usambazaji wa bidhaa zake utaendelea kuwa thabiti kupitia mtandao wake wa maghala 25 yaliyopo nchini kote.
“Tanzania ni nchi kubwa na yenye mahitaji tofauti na hivyo, upatikanaji wa nishati hii ni kipaumbele kikubwa kwetu sisi,” ameeleza meneja huyo.
Ameongeza, “Tumewekeza katika miundombinu inayotuwezesha kusambaza gesi ya kupikia sehemu mbalimbali nchini Tanzania.”
Kampuni ya Taifa Gas imesema, inaendelea kuzingatia vipaumbele vya kitaifa vya nishati pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Rostam Aziz, imeuhakikishia umma, kwamba bidhaa zake zitapatikana kwa wakati na kwa bei rafiki kwa mtumiaji.
Taifa Gas ni kampuni ya nishati ya Tanzania inayojihusisha na usambazaji wa gesi ya majumbani (LPG).
Gharama za gesi na mafuta zimepanda ulimwenguni, kufuatia kuongezeka kwa mvutano na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyoingia mwezi wake wa pili wiki hii.
ZINAZOFANANA
Hapa ndipo Mabingwa wanazaliwa, karibu Big Bounty Challenge
Airtel Tanzania yamkabidhi mshindi gari la Mazda CX-5
Gates of Love kuja imesheheni upendo na zawadi zisizoisha