William Lukuvi
MBUNGE wa zamani wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto, amemtaja hayati William Lukuvi, aliyefariki dunia leo asubuhi (tarehe 25 Machi 2026), kwamba ndiye aliyemungiza bungeni. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
“Lukuvi ndiye aliyenishika mkono na kuniingiza kwenye ulingo wa kisiasa. “Kwa kweli Lukuvi anamchango mkubwa kwenye safari yangu ya kisiasa. Naweza kusema yeye ndiye aliyeniingiza kwenye siasa na akanishauri nigombee uongozi wa vijana mkoa wa Iringa,” anasimulia.
Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, amefariki dunia,
leo Jumatano, katika hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.
Ndivyo taarifa ya serikali iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, ilivyoeleza kuhusiana na msiba huo.
Mbunge huyo wa Ismani, mkoani Iringa, alifikishwa hospitalini hapo kwa matibabu ya shinikizo la moyo.
Mwamoto anasema, aliyekuwa mbunge wa Ismani, kwa takribani miaka 30 (1995-2026), alimfahamu tangu akiwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM).
“Lukuvi alikuwa kama kaka yangu pamoja na kwamba sote tulikuwa wabunge. Mara zote alikuwa akinishauri na kuniongoza,” anaeleza.
Anaongeza, “Tumempoteza mtu ambaye hatuwezi kumsahau. Alikuwa mkweli na alikuwa na msimamo; akikona kitu hakiko sawa, alikuwa hasiti kukuambia ukweli.”
Naye mbunge wa sasa wa Kilolo, Ritta Kabati, akimzungumzia mwanasiasa huyo, ameeleza kuwa Lukuvi alikuwa kiongozi na alimchukulia kama baba yake mzazi.
“Siyo mimi tu, wabunge wote wa Iringa, tulimchukulia Lukuvi kama baba yetu.
Mwenyekiti huyo wa wabunge wa mkoa wa Iringa, anaeleza kuwa “…nimepatwa na mshtuko mkubwa na kwa kweli, mkoa wa Iringa na taifa, limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Lukuvi.”
Anasema, “Hatujategemea kama leo tutaamka tupate msiba mkubwa kama huu, Lukuvi anamchango mkubwa kwenye maendeleo ya mkoa wetu na kwa uzoefu wake, alikuwa ni kiuongo muhimu hapa bungeni.”
Anasema, “Sisi kama wabunge wa Iringa alikuwa kama Baba yetu tukipata jambo lolote tunamuita yeye; kuna vitu anatushauri. Tumepigania vitu vya maendeleo kwa pamoja kama timu na kusema kweli tumepata pigo kubwa sana.”
Wakati wa uhai wake, Lukuvi aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini, ikiwamo Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), mkuu wa mkoa na mshauri wa Rais, masuala ya siasa.
Alikuwa akitambulika na wenzake, kuwa mmoja wa wabunge wa muda mrefu kuliko wote waliokuwamo kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
William Vangimembe Lukuvi (70), alizaliwa tarehe 15 Agosti 1955, huko Mapogoro, mkoani Iringa.
ZINAZOFANANA
Mipango mbioni kuanzisha kituo cha Kimataifa cha huduma za kifedha nchini
William Lukuvi afariki dunia
Netanyahu achezea kipigo, aomba msaada mataifa mengine