Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Emmanuel Nchimbi
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi ameungana na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli yaliyofanyika Chato mkoani Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Katika ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwa ajili ya kumuenzi kiongozi huyo, Nchimbi amesema kuwa Hayati Magufuli alikuwa mfano wa uongozi thabiti uliotanguliza mbele maslahi ya taifa, akisisitiza kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ameeleza kuwa Magufuli alijitofautisha kwa kusimamia uwajibikaji, nidhamu ya kazi pamoja na kufanya maamuzi magumu yaliyolenga kuimarisha uchumi na huduma za kijamii nchini.
Nchimbi amebainisha kuwa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” itaendelea kuwa dira muhimu kwa Watanzania katika kujenga taifa lenye maendeleo.
Aidha, amewataka viongozi na wananchi kuendelea kuenzi mema aliyoyaacha Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwa wazalendo na kutumia vyema rasilimali zilizopo nchini kwa manufaa ya wote.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, dini pamoja na wananchi wengi waliokusanyika kumkumbuka na kumuombea Hayati John Mgufuli, wakieleza namna alivyoacha alama kubwa katika historia ya Tanzania.
ZINAZOFANANA
Jesca Magufuli: Uwezo wa kiongozi unapimwa kwa alama alizoacha
Meli kubwa nne za mizigo kufungua fursa Ziwa Tanganyika
Serikali yajipanga kutatua changamoto za mazingira ya biashara