March 16, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yajipanga kutatua changamoto za mazingira ya biashara

 

SERIKALI kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) mesema kuwa imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika mazingira ya biashara nchini ili kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha tatu cha Kikundi kazi cha mazingira ya biashara cha baraza hilo la biashara kilichofanyika jana katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau kutoka Serikalini pamoja na sekta binafsi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye ulemavu, Dk. Jim Yonazi, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili kwa pamoja changamoto zinazoikabili sekta ya biashara na kutafuta suluhisho la pamoja.

Alisema Serikali inaendelea kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto zinazokwamisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini, hivyo kikao hicho ni fursa muhimu kwa wadau wa biashara kutoka sekta mbalimbali kuainisha maeneo wanayoona yana changamoto ili yaweze kufanyiwa kazi zaidi.

“Tumejadili baadhi ya maeneo ambayo ni vikwazo kwa biashara, kama vile hoja ya punguzo la kodi iliyotolewa na wadau wa sekta binafsi, upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiriamali wa biashara ndogo ndogo pamoja na mapendekezo ya maboresho katika sekta ya afya,” alisema Dk. Yonazi.

Aliongeza kuwa, akiwa kama Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho, amewaagiza wajumbe kutoka sekta husika kulifanyia kazi suala hilo kwa undani ili kuja na mapendekezo yatakayowasilishwa katika kikao kijacho kwa ajili ya hatua zaidi.

Aidha, alibainisha kuwa malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wafanyabiashara wakubwa na wajasiriamali wadogo, ili kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na biashara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kikundi Kazi hicho kutoka sekta binafsi, Innocent Minja, kupitia wasilisho lake kwa wajumbe wa mkutano huo, alisema utafiti walioufanya umebaini changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo katika kuwavutia watu kufanya biashara na kukuza mitaji yao na kuhitaji kufanyiwa kazi kwa haraka.

“Tunapendekeza Serikali, pamoja na mambo mengine, ipunguze viwango vya kodi ili wafanyabiashara wengi waweze kumudu kufanya biashara na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Amesema kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, imebainika kuwa Tanzania inakuwa kiwango kikubwa cha kodi cha asilimia 18, ukitofautisha na nchi nyingine, hali inayokatisha tamaa kwa baadhi ya watu kufanya biashara na wengine kushawishika kuwekeza katika nchi nyingine.

Aliongeza kuwa ni muhimu pia Serikali kusimamia upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wfanyabishara hasa wadogo wadogo ili kukuza mitaji yao na kuongeza soko la ajira.

“Serikali pia inapaswa kuendelea kupima na kurasimisha ardhi ili wananchi waweze kuitumia kama dhamana wanapohitaji mikopo kutoka katika taasisi za fedha kama mabenki. Wananchi wengi wanashindwa kupata mikopo kutokana na kukosa dhamana,” alisema Minja.

Pia alitoa pendekezo la uwiano wa kodi, ambapo baadhi ya wafanyabishara, akitolea mfano wa maduka ya Kariakoo wanalipa kodi, huku wachuuzi wakiwa nje ya maduka wakifanya biashara hizo hizo lakini hawalipi kodi.

“ Hii inawafanya wafanyabishara wakubwa kufanya udanganyifu, ikiwemo kuwapa watu bidhaa zao wafanye kama wanavyofanya wamachinga ili na wasilipe kodi,” amesema.

Hata hivyo, aliwahakikishia wawekezaji na wadau wa sekta binafsi kuwa na imani na kikundi kazi hicho, akisema kitaendelea kuwasilisha changamoto zote zinazowakabili ili zifanyiwe kazi na Serikali, kwani kupitia majukwaa kama hayo changamoto nyingi zinapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC na Katibu wa Kikundi Kazi hicho, Dk. Godwill Wanga, alisema kikundi kazi hicho kitaendelea kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali katika sekta hiyo ya biashara.

Alisema kuwa hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo kukabiliana na adha ya ukosefu au kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati.

“Kikundi kazi hiki kitafanya utafiti na kuja na mapendekezo kuhusiana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati ili kuhakikisha haitaleta athari katika shughuli zetu za kiuchumi hapa nchini,” alisema Dk. Wanga.

Naye Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk. Blandina Kilama, alisema Serikali itaendelea kupokea maoni ya wadau mbalimbali wa biashara ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa takribani asilimia 70 ya uwekezaji hutoka katika sekta binafsi, ambayo pia imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa na kutoa ajira kwa Watanzania wengi.

“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa, kwani imeajiri Watanzania wengi na kuendelea kuchochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi,” alisema Dk. Kilama.

About The Author

error: Content is protected !!