March 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ALAF yaadhimisha Siku ya Wanawake kwa uzinduzi wa programu ya uongozi na kuisaidia jamii

 

KAMPUNI ya ALAF, inayoongoza katika suluhisho la paa na vifaa vya ujenzi Tanzania, imezindua Kundi la 5 la Mpango wa Wanawake katika Uongozi kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambayo iliadhimishwa Machi 8 duniani kote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uzinduzi huo, uliofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Jumatatu, ukiongozwa na kaulimbiu ya ‘Toa Upate’ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Tawala Msaidi wa Mkoa wa Dar es Salaam-Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Zubeda Masoud.

Uzinduzi huo pia ulikwenda sambamba na wafanyakazi kutambua mafanikio ya wanawake, huku wakionyesha dhamira yao ya uongozi, uwezeshaji na kuisaidia jamii.

Masoud aliupongeza uongozi wa ALAF kwa kuwapa wanawake umuhimu unaostahili na kuhakikisha wanashika nafasi za juu za uongozi katika kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kushiriki nao pamoja katika Siku ya Wanawake.

“Makampuni mengine yanatakiwa kuiga mfano huu wa ALAF kwani huu ni muendeleo mzuri wa kuadhimisha siku ya wanawake duniani,” alisema huku akiipongeza kampuni hiyopia kwa kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalumu ambao walikabidhiwa viti 10 vyenye magurudumu.

Akizingumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ALAF, Bibhu Nanda, aliyewakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo, Sateesh Yamsani, alisema kampuni itaendelea kuunga mkono mipango ya wanawake kama mpango wa wanawake katika uongozi ili kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata nafasi za uongozi ndani ya

ALAF na kwamba huu unakuwa mpango endelevu ili ALAF iendelee kishika nafasi ya juu katika sekta ya Viwanda kama mwajiri Bora. “Tumeona matunda ya mpango huu ulioanza miaka minne iliyopita na kama kampuni tutahakikisha kwamba unakuwa endelevu ili wanawake wengi zaidi waweze kushika nafasi hizi muhimu,”alisisitiza.

Naye Meneja Rasilimali Watu Msaidizi, Rehema Amry alisema: “Huu ni mpango unaolenga kuimarisha uwezo wa uongozi na kusaidia ukuaji wa kitaaluma wa wanawake ndani ya kampuni.”

Alisema maadhimisho ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee kwani ALAF inaadhimisha miaka 65 ya ubora, ubunifu na mchango katika maendeleo ya viwanda Tanzania. “Katika miongo sita iliyopita, kampuni imeendelea kukuza ukuaji jumuishi na kutoa fursa kwa watu wake na jamii inayowahudumia,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Amry, ALAF inapoendelea na safari yake ya ukuaji na matokeo yake chanya kwa jamii, inathibitisha dhamira yake ya kujenga mahali pa kazi shirikishi, ambapo wanawake wanawezeshwa kuongoza, kuhamasisha, na kuchangia katika maisha bora ya baadaye.

“ALAF, tunaamini kwamba kuwawezesha wanawake na kuzisaidia jamii zetu kunakwenda sambamba. Tunaposherehekea miaka 65 ya ubora, tunaendelea kujitolea kutengeneza fursa kwa wanawake kuongoza, huku tukifanya mabadiliko ya muhimu katika jamii. Hakika, hisani huanzia nyumbani.”

Wakati huo huo, katika ari ya kutoa kwa jamii, wafanyakazi wanawake ALAF walichangia kwa hiari kusaidia ajenda ya kampuni ya uwajibikaji kwa jamii.

Kwa juhudi zao za pamoja, viti 10 vya magurudumu vilitolewa kwa watoto wenye mahitaji maalumu, huku kiti kimoja cha magurudumu kikikabidhiwa kwa mfanyakazi wa ALAF, na kusisitiza imani kwamba hisani huanzia nyumbani.

Leo, ALAF, ambayo ilianza kazi Tanzania mwaka 1960, inatoa vifaa vya ujenzi ambavyo ni pamoja na bidhaa za paa zilizopakwa rangi ya awali na ‘alu-zinc’, mabomba, bidhaa za chuma na kutengeneza vifaa mbalimbali vya ujenzi.

About The Author

error: Content is protected !!