March 9, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mojtaba Khamenei ndiye mrithi wa Ayatollah Ali Khamenei, Iran

 

BARAZA la Wataalamu la Iran limemtangaza Mojtaba Khamenei, mwana wa marehemu Ayatollah Ali Khamenei, kuwa kiongozi mkuu mpya wa nchi hiyo. Tangazo hilo, limetolewa jana Jumapili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mojtaba aliyejenga uhusiano wa karibu na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, amechukua nafasi ya baba yake, anatajwa kuwa na msimamo mkali zaidi kuhusu Marekani kuliko hata baba yake.

Mojtaba Khamenei ametangazwa kiongozi mkuu mpya wa Iran, wakati Israel na Marekani wakiendeleza mashambulizi dhidi ya maghala ya mafuta ya Iran, huku milipuko ikionekana katika mji mkuu -Tehran.

Baraza la Wataalamu la Iran limemteua mwana wa kiongozi aliyeuawa, Ayatollah Mojtaba Khamenei – siku tisa baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel kumuua Ayatollah Ali Khamenei na kulitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati katika vita.

Mojtaba Khamenei, mwenye umri wa miaka 56, “ameteuliwa na kutangazwa kuwa kiongozi wa tatu wa mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa msingi wa kura ya maamuzi ya wawakilishi waheshimiwa wa Baraza la Wataalamu,” baraza hilo lilisema katika taarifa.

Lilisema pia kwamba halikusita “hata kwa dakika moja” kuchagua kiongozi mpya licha ya kile lilichokiita “uchokozi wa kikatili wa Amerika ya kihalifu na utawala mbaya wa Kizayuni.”

Rais wa Marekani Donald Trump hapo awali alimpuuza Khamenei mdogo akimwita “mtu dhaifu asiye na uzito mkubwa,” na Jumapili alisisitiza tena kwamba anapaswa kuwa na sauti katika uteuzi wa kiongozi mpya.

“Kama hatapata idhini kutoka kwetu hatadumu kwa muda mrefu,” aliiambia ABC News kabla ya tangazo hilo kutolewa.

Lakini mwanadiplomasia mkuu wa Tehran alisema Jumapili kwamba uamuzi huo ni wa Iran pekee, akiongeza kuwa “hatutaruhusu mtu yeyote kuingilia mambo yetu ya ndani.”

Akizungumza kwenye kipindi cha NBC “Meet the Press,” Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi alimtaka Trump awaombe radhi watu wa eneo hilo kwa kuanzisha vita.

Khamenei mdogo anachukuliwa kuwa mwanasiasa mwenye msimamo mkali wa kihafidhina, hasa kutokana na uhusiano wake na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guards), tawi la kiitikadi la jeshi la Jamhuri ya Kiislamu.

Jeshi la Israel hapo awali lilikuwa limeonya kwamba mrithi yeyote wa Khamenei “hatutasita kumlenga.”

About The Author

error: Content is protected !!