March 9, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

RITA yatoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa jengo la kituo cha watoto wenye uhitaji Dar

 

WAKALA wa Ufilisi na Udhamini (RITA) umekabidhi vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kuboresha mazingira bora ya makazi na elimu katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Huruma Children’s Home kilichopo jijini hapa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA, Irine Resuile amesema kuelekea siku ya wanawake duniani, RITA imeendelea kutekeleza sera yake ya kurudisha kwa jamii ambapo kila mwaka taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa jamii ikiwemo katika kituo hicho.

Katika sehemu ya msaada huo, RITA , pamoja na mambo mengine, imekabidhi mchanga,kokoto,magodoro,vyakula pamoja na mahitaji muhimu mengine muhimu.

“Watoto hawa ni kama watoto wengine tulionao majumbani, ambao pia wanastahili kupewa haki zao zote ikiwa ni pamoja na kusaidiwa katika mahitaji yao muhimu ya kila siku. Hivyo, sisi kama RITA tunatamani kuona ustawi mzuri wa watoto hao ambao ni sehemu ya taifa la kesho,” alisema Lesuile.

Aidha, alisisitiza kuwa taasisi ya RITA itaendelea kuwashika mkono watoto wote wenye uhitaji kwa kadri watakavyoweza na watahakikisha wanawafikia watoto wenye uhitaji katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi na mlezi wa kituo hicho, Dibogo Kitang’wa ameishukuru RITA kwa msaada walioutoa, kwani kukamilika kwa jengo hilo kutaenda kusaidia kuongeza idadi ya kupokea watoto katika kituo hicho, hususani wa jinsia ya kiume, ambao wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali za mtaani na kuwaweka katika mazingira hatarishi.

Amesema kituo hicho kimekua kikipata maombi mengi ya kupokea watoto wa jinsia ya kiume, lakini wanashindwa kuwapokea kutokana na uhaba wa sehemu za malazi na ndio sababu ya kuamua upanuzi wa kituo hicho ili kuwafikia wote wenye uhitaji.

“Tunaishukuru sana RITA kwa msaada huu na kuwaomba wadau wengine kutusaidia katika kumalizia ujenzi wa jengo hili na kuwafikia watoto wengi zaidi,” alisema Kitang’wa.

Ameongeza ku jengo hilo kwa sasa linahitaji kuwekewa miundombinu ya umeme na maji, lakini wamekosa pesa ikiwemo ya mahitaji ya vifaa na malipo ya kazi kwa mafundi ujenzi.

Aidha Kitang’wa alielezea maendeleo ya ujumla ya watoto hao nakusema kuwa wako katika hali nzuri na wanafurahia maisha yao, kwani kituo hicho kinapambana kuhakikisha wanapewa mahitaji yao muhimu kama elimu ili kutimiza ndoto zao maishani.

“Tunao vijana ambao wanasoma shule za awali, msingi , sekondari na vyuoni, ambao ni tegemezi katika taifa. Hivyo, tunaamini wataweza kujiajiri au kuajiliwa ili kuwa sehemu ya wachangiaji uchumi wa taifa,” alisema Kitang’wa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, mwakilishi Zainab Masilamba ameipongeza RITA kwa namna inavyojitoa kusaidia jamii zenye uhitaji na kuomba taasisi na makampuni mengine kuiga mfano huo.

About The Author

error: Content is protected !!