Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Dk. Lazarus Chakwera
HATIMAYE Serikali ya Tanzania, imekubali kumruhusu Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Dk. Lazarus Chakwera, Rais wa zamani wa Malawi, kuingia nchini kufanya uchunguzi wa mauaji ya 29 Oktoba mwaka jana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa ya jumuiya hiyo, iliyotolewa jana Jumamosi, tarehe 7 Machi 2026, imeeleza kuwa Serikali jijini Dar es Salaam na Dodoma, imekubali kumruhusu Dk. Chakwera, “kuingia nchini na kufanya kazi aliyotumwa.”
Dk. Chakwera, aliteuliwa na katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola, kufanya uchunguzi wa matukio ya 29 Oktoba mwaka jana na kisha kuanzisha “mchakato wa maridhiano,” chini ya usimamizi wa jumuiya hiyo.
Awali alipanga kuanza ziara ya siku nne nchini kuanzia tarehe 18 hadi 21 Novemba, ikiwa na lengo la kuanza majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya jumuiya hiyo, serikali ya Tanzania, ilimzuia Dk. Chakwera kuingia nchini kwa maelezo kuwa imeunda tume yake ya uchunguzi.
Katika ziara ya sasa, Dk. Chakwera atakutana na viongozi wa serikali, wanasiasa, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini na mila, pamoja na wadau wa kitaifa na kimataifa.
Mazungumzo hayo yanapania kuanzisha mjadala jumuishi kuhusu maridhiano, haki za kisiasa na kuimarisha demokrasia nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Jumuiya ya Madola, Prof. Paramagamba Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), ameieleza jumuiya hiyo, kuwa serikali ya Tanzania imeridhia kumruhusu mjumbe wake huyo, kufanya kazi nchini.
“Jumuiya ya Madola, imeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuchukua hatua zinazohitajika ili kuunga mkono ahadi yake iliyotajwa kwenye mkataba wa Jumuiya ya Madola na maadili yake ya kisiasa.
“Jumuiya imeamua kuiweka Tanzania katika ajenda yake rasmi na kuihimiza Serikali, kwa usaidizi wa Sekretarieti, kuruhusu kufanyiwa kazi maeneo yaliyoainishwa katika mkutano wa Sabini na Moja wa CMAG wa Desemba 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Imeongeza, “CMAG ilikaribisha ahadi ya Tanzania ya kupokea na kuwezesha ziara na kazi za Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu, Machi mwaka huu. CMAG inatarajia tathimini thabiti kutoka kwa Mjumbe Maalum na haswa kuhusu masuala yaliyoibuliwa na mkutano mkuu.”
Akizungumza uteuzi wa Dk. Chakwera, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, alisema uongozi na uzoefu wa rais huyo wa zamani wa Malawi, vitakuwa muhimu katika kuweka msingi wa majadiliano ya kujenga kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema, ana imani kuwa mchango wa Dk. Chakwera utaimarisha amani na uthabiti nchini Tanzania, kwa kuzingatia maadili ya Jumuiya ya Madola kama vile ushirikishwaji, uwazi, haki na uwajibikaji.
ZINAZOFANANA
UNDP, Uingereza watoa 70mil kuimarisha Biashara Bunifu za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
Mojtaba Khamenei ndiye mrithi wa Ayatollah Ali Khamenei, Iran
RITA yatoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa jengo la kituo cha watoto wenye uhitaji Dar