KANISA Katoliki Jimbo la Musoma, limefutangaza barua yake iliyokuwa imeruhusu Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), kutumia uwanja wake, kwa ajili ya Siku ya Wanawake Duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Barua kutoka kwa mkurugenzi wa kituo hicho, Padre Michael Nyamhanga, kwenda kwa katibu mkuu wa Bawacha, inaeleza kuwa uamuzi wa kutengua ruhusa hiyo, umetokana na kile ilichoita, “sababu zilizopo nje ya uwezo wa Kanisa.”
Kwa mujibu wa Padre Nyamhanga, Kanisa Katoliki limeamua kuchukua hatua hiyo, kutokana na sintofahamu iliyoibuka kati ya waandaaji wa tukio hilo na Jeshi la Polisi nchini.
Wanawake wa Chadema nchi mzima, walipanga kukusanyika mjini Musoma, kufanya maadhimisho ya kilele cha sherehe za Siku ya Wanawake Duniani. Sherehe hizo, zilitarajiwa kufanyika katika uwanja wa Matumaini uliyopo Musoma, mkoani Mara.
Kilele cha sherehe ya siku ya Wanawake ulimwenguni, zinahitimishwa Jumapili ya tarehe 8 Machi ya kila mwaka.
Amesema, “Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tunasikitika kutengua barua yetu na hii ni kutokana na sintofahamu iliyopo kati yenu na Jeshi la Polisi Tanzania, ambapo sisi hatuwezi kuingilia kati kwa namna yoyote ile.”
Uamuzi wa kanisa umekuja siku chache baada ya Jeshi la polisi mkoani Mara, kutangaza kuzuia kufanyika kwa maadhimisho hayo, kwa madai kuwa Chadema, kimezuiwa na Mahakama kufanya shughuli za kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alidai kuwa kitendo cha Chadema kuandaa maadhimisho hayo, ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya mahakama inayokizuia chama hicho kujihusisha na shughuli za kisiasa hadi kesi ya msingi itakapomalizika mahakamani.
Alisema, jeshi la Polisi linaendelea kuitambua amri hiyo ya mahakama iliyotolewa tarehe 10 Juni 2025, kwa kuwa bado haijabatilishwa wala kutenguliwa na mahakama yoyote nchini.
Wakati hayo yakiendelea msafara wa Bawacha kutoka mkoa wa Kagera uliokuwa ukielekea Musoma kwa ajili ya kushiriki maadhimisho hayo, umezuiwa na polisi majira ya saa 8 usiku, mjini Geita.
Jumla ya watu 51 waliokua kwenye msafara huo wamekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Geita.
Hali kama hiyo, imewakuta Bawacha wa majimbo ya Kinondoni na Kawe, waliokuwa wakitumia mabasi mawili ya mkoa wa kichama wa Kinondoni, waliokamatwa maeneo ya Mlandizi mkoani Pwani.
Msafara mwingine wa wanawake wa Segerea, umefanikiwa kupenya mitego hadi kuingia mkoani Dodoma, ingawa kuna uwezekano mkubwa nao wakakamatwa mbele ya safari.
MwanaHALISI Online linaendelea kufuatilia misafara ya BAWACHA nchi mzima, na hatua kwa hatua, ili kuwafamisha wasomaji wake kinachoendelea.
ZINAZOFANANA
Waziri wa Fedha awaongoza wateja, wadau wa NBC futari maalum Dar
BAKWATA: Wapuuzeni wanaokashifu Uislamu
Hatma ya kesi ya mgawanyo wa mali za Chadema leo