March 6, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waziri wa Fedha awaongoza wateja, wadau wa NBC futari maalum Dar

 

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, jana aliwaongoza baadhi ya Waislamu jijini Dar es Salaam kushiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa ajili ya wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika hafla hiyo, Waziri huyo alizikumbusha taasisi za fedha nchini wajibu wao katika kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi wa kisasa unaochochewa na uwekezaji, viwanda, biashara pamoja na ubunifu wa kidijitali.

Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo, wakiwemo viongozi wa serikali na viongozi wa dini. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, aliwaongoza viongozi na maofisa wengine wa benki hiyo kuhudhuria hafla hiyo, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Omar aliishukuru na kuipongeza NBC kwa kuandaa tukio hilo la kiimani, akisisitiza umuhimu wa uthabiti wa sekta ya fedha katika kukuza uchumi wa taifa. Alieleza kuwa ili kufanikisha uthabiti huo, ni lazima taasisi za fedha zijenge uaminifu mkubwa kwa wateja wao, huku akitaja matukio yanayogusa imani za wateja kama njia muhimu ya kuimarisha mahusiano hayo.

“Hii ndiyo sababu tunazithamini sana taasisi za fedha zinazojenga ukaribu zaidi na wateja pamoja na wadau wake muhimu. Tunaamini kwamba uaminifu ndio msingi wa mzunguko wa fedha katika uchumi, kama ilivyo kaulimbiu yenu ya ‘Daima Karibu Nawe’. Nawapongeza sana NBC kwa kuendeleza utamaduni huu,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea uzalishaji wa ndani, hivyo taasisi za fedha zina wajibu mkubwa wa kuunga mkono juhudi hizo.

“Nyote mnafahamu kuwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ni kujenga Tanzania yenye uchumi wa kisasa unaochochewa na uwekezaji, viwanda, biashara na ubunifu wa kidijitali. Ili kufikia malengo haya, sekta ya fedha hasa benki zina jukumu la msingi — si tu kutoa huduma za kifedha bali pia kuwa wawezeshaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi,” alisisitiza.

Aidha, alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa taasisi za fedha ili ziweze kutoa mchango unaoendana na matarajio ya dira hiyo.

“Tuendeleze amani, upendo na ushirikiano ili kutimiza malengo yetu ya pamoja ya maendeleo,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, alisisitiza dhamira ya benki hiyo kuendeleza utamaduni wa kuandaa matukio kama hayo kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na wadau wake. Alieleza kuwa NBC inatambua mchango mkubwa wa wadau wake muhimu, wakiwemo serikali na wateja, katika mafanikio ya shughuli zake.

Alibainisha kuwa wateja wa benki hiyo ni mabalozi muhimu wanaotangaza ubora wa huduma zinazotolewa na NBC kwa jamii.

“Tunatambua pia nafasi ya Mwenyezi Mungu katika kutuwezesha kuendesha taasisi zinazogusa ustawi wa maisha ya watu kama hizi. Ndiyo maana tumekuwa tukitoa wito kwa wananchi kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa, kwa sababu weledi na ufanisi wao katika uongozi hutegemea baraka na muongozo wa Mwenyezi Mungu,” alisema.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alishukuru ushirikiano unaoendelea kati ya benki hiyo na wadau wake mbalimbali, wakiwemo Serikali, viongozi wa dini pamoja na wateja wake wakubwa na wadogo.

Alieleza kuwa kupitia ushirikiano huo, NBC imefanikiwa kubuni na kutoa huduma mbalimbali za kifedha zinazozingatia misingi ya Kiislamu, zikiwemo akaunti za akiba na biashara, akaunti za uwekezaji wa muda maalum (Fixed Investment Accounts), pamoja na huduma za uwezeshaji wa kifedha kupitia mfumo wa Murabaha. Pia alitaja huduma ya Rariba, inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, pamoja na suluhisho la kifedha kwa wateja binafsi na wa kibiashara.

“Kupitia huduma hizi zinazozingatia misingi ya Kiislamu, zaidi ya wateja 43,000 wanahudumiwa kupitia dirisha hili, wakiwa na amana zinazozidi shilingi bilioni 80, huku uwezeshaji wa kifedha uliotolewa kupitia dirisha hilo ukizidi shilingi bilioni 46. Tunawahamasisha wateja na wadau wengi zaidi kuendelea kutumia huduma hizi,” alisema.

Aidha, Sabi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa ukuaji wa sekta ya fedha na biashara nchini. Pia aliipongeza Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha uliosaidia kuimarisha mifumo ya kifedha nchini.

“NBC tunaendelea kuwa na dhamira ya kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuwezesha sekta ya fedha kuchochea shughuli za uzalishaji, kusaidia biashara ndogo, za kati na kubwa, na kuongeza ujumuishi wa kifedha kupitia mifumo ya kidijitali pamoja na huduma zinazozingatia imani za kidini,” alisisitiza.

About The Author

error: Content is protected !!