ABUBAKAR Zubeir Bin Ally, Mufti na Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), amewataka waumini wa dini ya Kiislamu nchini, viongozi na Watanzania kwa ujumla, kuwapuuza wanaoeneza chuki za kidini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari, wakati akisoma tamko la maazimio ya kikao cha Baraza la Ulamaa, kilichofanyika tarehe 4 Machi 2026, makao makuu ya baraza hilo, amehimiza umuhimu wa kuendelea kuishi kwa upendo, umoja na kuvumiliana kama yalivyo mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Muft wa Bakwata amewasihi Waislamu kutokubali kuchokozeka na watu wachache wanaochapisha jumbe za kumtukana Mtume, kuukashifu Uislamu na kuibeza dini hiyo.
“Tunaamini kuwa wanaofanya hayo sio wakristo wala watu wa dini nyingine yeyote bali watu hao wana nia ovu ya kutuchonganisha ili tugombane na kutia mtafaruku kati yetu na dini nyingine na jamii kwa ujumla,” ameeleza.
Aliongeza, “Niwasihi Waislamu wasiingie kujibizana kwasababu watu hao wanataka kueneza chuki na fitna dhidi ya dini nyingine.”
Aidha, Sheikh Zubeir amewaomba waislamu wote nchini, masheikh, wanazuoni, maustadh, maimamu na waalimu wa dini, pamoja na jamii kwa ujumla, kuendelea kuishi kwa upendo, kuvumiliana, kustahimiliana na kulinda umoja wa kitaifa uliodumu kwa muda mrefu.
“Mtume Muhammad (S.A.W) aliishi na wasiokuwa waislamu kwa wema na aliamiliana nao kwa wema,” amefafanua.
Katika hatua nyingine, Mufti Zubeir ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kufuatia maelekezo ya serikali juu ya magonjwa ya Uviko-19, homa ya ini, dengue na kipindupindu.
Amewatakia pia muendeleo wa mfungo mwema waumini wote wa dini ya Kiislamu wanaoendelea na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
ZINAZOFANANA
Waziri wa Fedha awaongoza wateja, wadau wa NBC futari maalum Dar
ATCL yaandaa safari maalum kuwarejesha Watanzania waliopo Dubai
Wanawake si washindani wa Wanaume – Balozi Zena