March 1, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ayatollah Ali Khamenei: Kiongozi Mkuu wa Iran athibitika kuawa

 

RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amefariki dunia, saa chache baada ya taifa lake na Israel kufanya mashambulizi makubwa nchini Iran. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Khamenei (86), aliuawa mapema Jumamosi asubuhi katika ofisi yake, iliyopo jengo la Leadership House, mjini Tehran, wakati akitekeleza majukumu yake.

Taarifa za kifo cha kiongozi huyo, zimethibitishwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na kuongeza kwamba, rais wake, mkuu wa mahakama na mmoja wa wanasheria wa Baraza la Walinzi – chombo chenye nguvu – watasimamia kipindi cha mpito kufuatia kifo cha Khamenei.

Picha za satelaiti, zilizothibitishwa na BBC Verify zilionyeshz kulikuwa na uharibifu mkubwa katika sehemu za jengo ambalo Khamenei alikuwapo.

Mapema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema makao ya Khamenei Tehran yameharibiwa katika “shambulio kali na la kushtukiza” na kwamba kuna dalili kwamba kiongozi huyo “hayupo tena.”

Kifo cha Khamenei kilitangazwa baadaye kwenye televisheni ya taifa ya Iran.

Iran ilijibu mashambulizi kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel na nchi nne za Kiarabu ambazo zina kambi za kijeshi za Marekani: Bahrain, Kuwait, Qatar na UAE.

Taarifa zinasema, jopo la Wataalamu wa Uongozi – Baraza la Maulama – sasa linatarajiwa kumteua mrithi wa Khamenei, jambo ambalo Katiba ya Iran inasema, “lazima lifanyike haraka iwezekanavyo.”

Hata hivyo, kufanyika kwa haraka kwa shughuli hiyo, wakati Iran inashambuliwa na Marekani na Israel kunaweza kuwa vigumu kutokana na sababu za kiusalama.

Khamenei mwenyewe aliteuliwa siku hiyo hiyo Ruhollah Ayatollah Khomeini alipokufa.

About The Author

error: Content is protected !!