MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla jana aliwaongoza baadhi ya waislamu visiwani humo kushiriki hafla fupi ya futari iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa ajili ya wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo visiwani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Hafla hiyo ilifanyika kwenye hotel ya Madinat Al Bahr, Zanzibar ikihusisha wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo wakiwemo viongozi wa serikali na dini akiwemo Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi. Mkurugenzi wa Idara ya Mikopo wa NBC, Saleh Mohammed alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na wafanyakazi wa benki ya NBC.
Pamoja na ushiriki huo, Abdulla aliishukuru na kuipongeza NBC kwa kuandaa tukio hilo la kiimani, akieleza kuwa ni ishara ya moyo wa kujali na kujenga mahusiano imara na jamii.
Alitoa shukrani za dhati kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutambua mchango wa NBC katika maendeleo ya visiwa hivyo—kuanzia msaada wa kifedha, ushauri wa kitaalamu, hadi ushiriki wake katika mipango mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
“Kushiriki futari kama hii pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wateja wenu ni jambo la heri, hususan katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Ni thamani kubwa kwenu kama waandaaji, kwetu kama walengwa, na mbele ya Mwenyezi Mungu pia… tunawashukuru sana,” alisema.
Aliongeza kuwa NBC imeendelea kujidhihirisha kama taasisi inayojitoa kwa dhati katika juhudi za kiimani na kimaendeleo, jambo lililomfanya kuupa kipaumbele mwaliko huo ili kufikisha shukrani zake binafsi na za serikali.

“Kupitia matukio kama haya, Wazanzibar wengi zaidi wanavutiwa kuwa karibu nanyi, si tu kibiashara bali kwa sababu mmeonesha kuwa uhusiano wenu na wateja ni zaidi ya miamala ya kibenki,” alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha ili ziweze kunufaika na ukuaji wa uchumi unaochochewa na miradi ya maendeleo pamoja na sekta muhimu kama utalii, biashara na uvuvi.
Kwa upande wake, Bw. Saleh Mohammed alisema kuwa kuandaa futari katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Zanzibar, ni sehemu ya utamaduni wa NBC unaolenga kuimarisha ukaribu na jamii.
Alieleza kuwa mafanikio ya benki hiyo, ikiwemo ongezeko la wateja mikoa mbalimbali pamoja na visiwani Zanzibar, yanatokana na mahusiano mazuri na utoaji wa huduma unaozingatia mahitaji halisi ya wateja, ikiwemo misingi ya kiimani.
Alitolea mfano huduma ya La’ Riba, inayowezesha wateja wenye imani ya Kiislamu kupata huduma za kifedha zinazoendana na misingi ya dini yao.
Sambamba na hilo, alibainisha kuwa NBC imeendelea kuboresha huduma za kidijitali ili kuwapa wateja urahisi zaidi, ikiwemo kufungua akaunti kwa njia ya mtandao, kufanya malipo ya serikali (GEPG), kununua umeme , pamoja na kulipa ankara mbalimbali kwa urahisi.
“Tunaendelea kuwaalika wateja wetu kutumia NBC Kiganjani App, NBC Connect, mashine zetu za POS na kadi zetu za malipo ili kufurahia huduma za kibenki zilizo salama, za haraka na za kisasa zaidi,” alisema.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa utoaji wa zawadi kwa wageni waalikwa na kutoa fursa ya kubadilishana mawazo, kuimarisha mtandao wa kibiashara na kijamii, pamoja na kusherehekea kwa pamoja katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
ZINAZOFANANA
‘Meli iliyokamatwa na Cocaine nchini El Salvador ilisajiliwa nchini’
NBC yakabidhi gari kwa Mshindi wa Kampeni ya Huduma za Kidigitali
Aspect Gaming & Superspade Games kuleta balaa kwa kasino mtandaoni Meridianbet