JAJI wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Deo John Nangela amejitosa katika kinyang’anyiro katika Uchaguzi wa Majaji Sita wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Baraza la Nchi Wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) linatarajia kufanya uchaguzi huo ambao, macho ya wadau wa sheria na diplomasia yanaelekezwa kwa karibu zaidi katika ushindani huo unaobeba uzito mkubwa wa kisiasa, kisheria na kimkakati duniani.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kwa uzito katika kinyang’anyiro hicho ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, hatua inayofungua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Tanzania katika uongozi wa taasisi za kimataifa za haki jinai.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika katika kikao cha 25 cha Baraza la Nchi Wanachama kinachotarajiwa kuanza tarehe 7 hadi 17 Desemba 2026, ukiwa sehemu ya mchakato wa mara kwa mara wa kuhuisha jopo la majaji 18 wa ICC wenye jukumu la kusimamia kesi nzito za uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uchokozi wa kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, uteuzi wa majaji wa ICC hauishii kuwa tukio la kitaaluma pekee, bali ni maamuzi yanayoathiri mizani ya haki na siasa za kimataifa.
Kuingia kwa jina la Nangela katika orodha ya wagombea kunatazamwa kama ishara ya kukua kwa ushawishi wa wataalamu wa sheria kutoka Afrika Mashariki ndani ya majukwaa ya kimataifa. Akiwa na Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Shahada ya Uzamili (LLM) kutoka SOAS University of London, pamoja na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wasifu wake unaakisi mchanganyiko wa uzoefu wa kitaifa na mitazamo ya kimataifa sifa inayozidi kupewa uzito katika mahakama za kimataifa.
Kwa mujibu wa mkataba wa Roma, hususan kifungu cha 36(3)(a), majaji wa ICC wanapaswa kuwa watu wenye maadili ya hali ya juu, uadilifu usiotiliwa shaka na uwezo wa kushika nyadhifa za juu za kimahakama katika nchi zao. Hata hivyo, tafsiri halisi ya masharti hayo mara nyingi imekuwa ikivuka taaluma ya sheria na kuingia katika eneo la diplomasia, ushawishi wa kikanda na uwakilishi wa kijiografia mambo yanayoifanya kila uchaguzi wa majaji kuwa pia uwanja wa siasa za kimataifa zisizoonekana wazi.
Ndiyo maana Baraza la Nchi Wanachama lilipitisha azimio ICC-ASP/22/Res.3 lililoanzisha mfumo wa kudumu wa uhakiki wa kina (vetting mechanism) kwa wagombea, likilenga kuimarisha uwazi na kuondoa malalamiko ya awali kwamba baadhi ya uteuzi uliathiriwa na misukumo ya kisiasa badala ya ubora wa kitaaluma. Mfumo huo mpya unatazamwa kama jaribio la kurejesha imani kwa ICC, ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kuhusu utekelezaji wa haki unaodaiwa kuathiriwa na siasa za kimataifa.
Iwapo Dk Nangela atafanikiwa kuchaguliwa, hatua hiyo haitakuwa mafanikio binafsi pekee bali pia ishara ya kuongezeka kwa mchango wa Tanzania katika mifumo ya haki ya kimataifa.
ZINAZOFANANA
Aliyemkamata mhamasishaji vurugu Mbeya atoa ushahidi kesi ya Lissu
Lissu alivyombana shahidi wa 14 wa serikali, neno kwa neno
Kardinali Pengo kuzikwa Pugu Feb 28