MAHKAMA Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali maombi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 yaliyohusu uwakilishi katika majimbo manane ya kisiwani Pemba. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Majimbo hayo ni Kiwani, Mkoani, Chake Chake, Chonga, Wawi, Wingwi, Micheweni na Kojani ambayo waliokuwa wagombea wa Chama cha ACT Wazalendo wanalalamika kuwa haki haikutendeka.
Katika uamuzi wake, Mahkama kupitia kwa Jaji Haji Khamis Suleiman, ilikubaliana na pingamizi zilizowekwa na upande wa walalamikiwa kuwa hati za viapo zilizoambatanishwa na maombi zilikuwa na kasoro nyingi za kisheria.
Jaji Haji akisoma uamuzi leo, alisema mahakama imejiridhisha kuwa kutokana na kasoro za kisheria, hati za viapo za walalamikaji katika mashauri hayo, haziwezi kutambuliwa wala kuwa sehemu ya maombi yaliyowasilishwa mahkamani.
Uamuzi huo ulitolewa mbele ya jopo la mawakili wa pande hizo mbili, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi Said Salim na wa ACT Wazalendo wakiwakilishwa na Mwanasheria Mkuu wake, Omar Said Shaaban.
Uamuzi huo umekuja chini ya wiki moja tangu Mahkama Kuu hiyo kupitia Jaji Salma Ali Hassan, kuyatupa maombi ya zuwio la kuteketezwa nyaraka za uchaguzi wa 2025 baada ya Tume ya Uchaguzi kutamka tarehe 3 Februari 2026 kuidhinisha uteketezaji wa nyaraka hizo. Maombi hayo yakihusu majimbo 17 ya kisiwani Unguja.
Hoja hizohizo zilitumika kufikiwa uamuzi huo unaotoka huku malalamiko ya msingi yakiwa hayajawahi kupewa nafasi ya kusikilizwa mahkamani. Ni kwa sababu kuemkuwa na mfululizo wa mapingamizi ya awali yanayowekwa na Wanasheria wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Uchaguzi Zanzibar [ZEC] ndio walalamikiwa kwenye mashauri hayo. Maombi mapya yalifunguliwa Ijumaa iliyopita kwenye Mahkama Kuu Tunguu lakini hayajapangiwa jaji wa kuyasikiliza.
Wakati maombi ya zuwio yanatupwa na kudhoofisha uhalali wa mashauri halisi 25 yaliyofunguliwa na ACT Wazalendo, Tume ya Uchaguzi juzi ilitangaza rasmi imeshateketeza nyaraka zilizotumika kisiwani Pemba, ikisimamia hoja yake kuwa imetekeleza kifungu 98[3] cha Sheria ya Uchaguzi Namba 1 ya mwaka 2018 kinachoelekeza hatua hiyo kuchukuliwa baada ya siku 90 kupita ulipofanyika uchaguzi iwapo hakuna katazo lolote la kisheria.
ZINAZOFANANA
Nilitwa Polisi kuhojiwa kama shahidi wa kesi ya Lissu
Kesi ya Lissu: Shahidi aeleza alivyomkamata aliyehamasisha vurugu za uchaguzi
EACOP yakabidhi karakana na vifaa vya mafunzo katika chuo cha Don Bosco