February 12, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu amaliza kumbana shahidi wa siri wa nne sasa amsubiri watano

Tundu Lissu akiingia mahakamani

 

SHAHIDI wa nne wa serikali ambaye ni shahidi wa siri aliyepewa utambulisho wa ‘P5’ kwenye kesi Na.19605 ya mwaka 2025 inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amemaliza kutoa ushahidi wake. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Leo tarehe 12 Februari mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akishirikiana na Jaji James Karayamaha na Jaji Ferdinand Kiwonde shahidi huyo aliongozwa na wakili wa serikali Ajuwaye Nzengeli kutoa ushahidi wake.

Katika ushahidi wake ‘P5’ aliiambia mahakama kuwa tarehe 4 April 2025, aliperuzi kwenye mtandao wa Facebook kupitia simu yake aina ya Sonny Experior Galaxy aliona video ya Lissu akisema kuwa kuwa uchaguzi wa 2025 hatafanyika atakinukisha.

Shahidi huyo amedai mahakamani hapo kuwa alivyoona video hiyo alipata hofu na kwamba aliona watu kwenye kijiwe cha kahawa wakiwa wamehamasika kufanya vurugu kwenye uchaguzi.

“Baada ya hapo mimi nikaona kuwa siku ya uchaguzi kutakuwa na fujo kubwa,”alidai P5.

Shahidi huyo aliyekuwa akisikika sauti yake bila yeye mwenyewe kuonekana akiwa kwenye kizimba cha shahidi wa siri alidai kuwa alimpigia simu ndugu yake ambaye ni askari na kumfahamisha jambo hilo ambalo yeye alidai aliona kuna hatari ya kufa njaa kwa kuwa kunaweza kutokea machafuko.

P5 alidai kuwa aliitwa Polisi kwa ajili ya mahojiano naye akatoa ushirikiano.

Baada ya kumaliza kuwasilisha ushahidi wake P5 . Lissu alianza kumuuliza maswali ya dodoso (cross- examination) ambapo alimuuliza yaliyotokana na ushahidi wake.

Lissu alimuuliza katika maelezo aliyoyatoa mahakamani Leo kwamba alipata njaa siku siku kutokana na vurugu za Oktoba 29 ndio aliyoyatoa tarehe 9 Aprili 2025 akajibu ndio .

Lissu alimuuliza maana ya kukinukisha shahidi akajibu ni kufanyika kwa vurugu, ndio Lissu alipotoa Kamusi ya Kiswahili Sanifu na kuieleza mahakama hiyo kuwa neno nukisha lina maana mbili linalotokana na mzizi nuka au nukia kwa maana ya nuka toa harufu mbaya na nukia toa harufu nzuri “wewe hiyo ya nukisha ni kufanya vurugu umeitoa wapi”.

Baada ya kumbana kwa maswali kwa takrani dakika 40 Lissu alihitimisha na kuieleza mahakama kuwa hana swali la ziada kwa shahidi.
Upande wa mashtaka nao haukuwa na swali za kusawazisha badala yake Wakili wa Serikali Mwandamizi Renatus Mkude akaiomba mahakama hiyo iaharishe kikao hicho mpaka saa nane kwa kuwa shahidi wao yupo njiani.

Jaji Ndunguru ameahirisha shauri hilo mpaka saa nane mchana.

About The Author

error: Content is protected !!