February 11, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

DED Yegella: Fedha za ndani kunufaisha kata zote Mbeya DC

 

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC), Erica Yegella, amesema kuwa mapato yote yatakayokusanywa kutoka katika vyanzo vya ndani vya Halmashauri yatatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zote 28 za wilaya hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Yegella ameyasema hayo jana tarehe 10.02.2026 wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Halmashauri ya Wilaya (DCC), kilichoketi kujadili na kupitisha Rasimu ya Mapendekezo ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha huo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh. 72.4 bilioni kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo mapato ya ndani na ruzuku kutoka Serikali Kuu. Fedha hizo zitagharamia mishahara, matumizi ya kawaida (OC), utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na vyanzo fungiwa kama ‘CHF’, ‘User Fee’, ‘NHIF’ na Michango ya Jamii.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema Watendaji wa Kata (WEOs) na Watendaji wa Vijiji (VEOs), kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kata na vijiji wakiwemo Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani, wamefanya kazi kubwa katika kuhakikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani yanafikiwa kama ilivyopangwa.

Aidha, ameongeza kuwa kupitia ushirikiano wa pamoja, Halmashauri imefanikiwa kudhibiti utoroshwaji wa mazao, ikiwemo kukamata magunia yaliyofungwa kwa mtindo haramu wa lumbesa yakitoka Halmashauri tunazopakana nazo.

“Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, tumeweza kukamata na kutoza faini mizigo iliyofungwa kwa mtindo haramu wa lumbesa kwa asilimia 228. Vilevile, mchakato wa uuzaji wa viwanja vya Tanganyika Packers umefikia asilimia 850, huku makusanyo ya vibali vya ujenzi yakifikia asilimia 14,” amesema Yegella.

Akisisitiza kuhusu fedha za miradi ya maendeleo, Yegella amesema kuwa mapato ya ndani yatapelekwa moja kwa moja kwenye kata husika. Mpango uliopo ni kuhakikisha kila kata inapatiwa Sh. 5 milioni, huku kipaumbele kikielekezwa kwenye kata ambazo hazijawahi kunufaika na fedha hizo hapo awali.

Ameongeza kuwa Halmashauri inaendelea kuimarisha mawasiliano na ufuatiliaji ili kuhakikisha kila fedha inayotolewa inatumika kikamilifu kwa lengo lililokusudiwa, kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Mbeya.

About The Author

error: Content is protected !!