February 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tanzania kujisogeza Ulaya, Zungu apiga hodi Serbia

 

WAKATI uhusiano wa Tanzania na mataifa ya Ulaya ukiyumba Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu amefanya mazungumzo ya kikazi na Spika wa Bunge la Serbia, Ana Brnabic, leo tarehe 10 Februari 2026 katika viwanja vya Bunge la Serbia Jijini Belgrade. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Duru zinaeleza kuwa ziara ya spika Zungu na viongozi wengine waandamizi wa kiserikali zinalenga kujenga upya uhusiano wa Tanzania na mataifa ya Ulaya.

Mazungumzo hayo yamekuja wakati mataifa yote mawili yakitafuta kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji na maendeleo ya taasisi za kibunge.

Serbia, yenye historia ndefu ya kuwa kiungo cha kisiasa na kiuchumi katika eneo la Balkans na Ulaya Mashariki, imeendelea kujijenga kama kitovu cha viwanda vya kati na teknolojia, jambo linaloifanya kuwa mshirika muhimu kwa Tanzania inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya mazao yake.

Katika ngazi ya kidiplomasia, uhusiano wa Tanzania na Serbia unajenga daraja jipya la ushirikiano wa Kusini na nchi za Ulaya ya Kati, ukiongeza sauti ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa.

Iwapo ushirikiano huo utaendelezwa kwa mikakati madhubuti, Tanzania inaweza kujijenga kama kitovu cha Serbia katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku Serbia ikawa daraja la Tanzania kuelekea masoko ya Balkans na Ulaya Mashariki.

Hatua hiyo si tu itachochea ukuaji wa uchumi na biashara, bali pia itajenga taswira mpya ya ushirikiano wa kimkakati unaovuka mipaka ya kijiografia na kuongeza ushindani wa mataifa hayo katika uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.

About The Author

error: Content is protected !!