February 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TAMISA yataja maeneo 20 muhimu ya ‘kupiga pesa’ kwenye madini

 

CHAMA cha Wasambazaji wa Bidhaa na Watoa Huduma Migodini (TAMISA) kimebainisha maeneo 20 muhimu ambayo Serikali imeyaainisha hivi karibuni kwa Watanzania waweze kushiriki kikamilifu na kunufaika na sekta ya madini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa, alisema kuwa mpango huo unalenga kufungua milango kwa Watanzania wanaojihusisha na shughuli za madini.

“Kwa mara ya kwanza katika historia, Serikali imetangaza rasmi orodha ya bidhaa na huduma 20 ambazo zitatolewa na kampuni zinazo milikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini nchini kupitia utoaji huduma mbalimbali,” alisema Kumalilwa.

Aliongeza kuwa lengo la Serikali na TAMISA ni kuhakikisha Watanzania wanapata faida za moja kwa moja kutokana na rasilimali zao kupitia ajira, zabuni, na fursa nyingine za kiuchumi zinazotokana na shughuli za migodi, kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya kitaifa ya Maudhui ya Ndani.

Baadhi ya fursa zilizotajwa ni utengenezaji wa vifaa vya ujenzi, kama vile saruji, nondo, na nyaya mbalimbali. Sekta nyingine zilizopatiwa kipaumbele ni utengenezaji wa vilainishi kwa ajili ya mitambo mikubwa na midogo, utengenezaji wa vilipuzi kwa ajili ya madini, huduma za kisheria, na huduma za usafirishaji na usambazaji (logistics).

“Sasa ni muda muafaka kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizi katika maeneo haya 20, kutoka kwenye usambazaji wa bidhaa hadi utengenezaji wa bidhaa hizo wenyewe,” alielezea Kumalilwa.

Hata hivyo, alikiri changamoto zinazopo katika utekelezaji wa sera ya Maudhui ya Ndani, akibainisha kuwa TAMISA inaendelea kupokea taarifa kuhusu baadhi ya migodi inayokiuka miongozo kwa kutoa zabuni kwa kampuni zisizo na umiliki wa Watanzania.

“Baadhi ya migodi haitumii wazabuni wa ndani kutoa vifaa na huduma muhimu, na wengine huweka masharti magumu yasiyoruhusu ushiriki wa ndani,” alibainisha Kumalilwa.

Uamuzi wa Serikali ulianza kutekelezwa rasmi tangu tarehe 15 Novemba 2025, kufuatia marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za Mwaka 2018 kupitia Kanuni ya 13A.

Kumalilwa pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipaumbele kilichopewa sekta ya madini, hususan kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata nafasi stahiki za usambazaji wa bidhaa na huduma chini ya sera ya Maudhui ya Ndani.

Aidha, alimpongeza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kwa kusimamia vizuri sekta ya madini na kuhakikisha Watanzania wananufaika na ukuaji wake.

“Tunampongeza sana Waziri kwa jitihada zake za kuharakisha ukuaji wa sekta ya madini na kuunda mazingira rafiki kwa Watanzania kushiriki kikamilifu, ikiwemo kupata nafasi za kutoa huduma na uwekezaji,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMISA, Japhet Mussa, alisema Serikali inatambua dhamira halisi ya Watanzania kushiriki kikamilifu katika biashara ya madini na iko tayari kuunga mkono jitihada za kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

“Tunahimiza Watanzania kuwekeza katika sekta ya madini. TAMISA, kwa kushirikiana na Serikali, imepewa ekari 125 eneo la Buzwagi mkoani Shinyanga kwa wawekezaji wa ndani kujenga viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya soko la madini,” alisema Mussa.

Aliongeza kuwa TAMISA, kwa kushirikiana na Serikali, iko tayari kulinda soko la bidhaa zinazotengenezwa na wawekezaji wa ndani, akibainisha kwamba hata sheria za uwekezaji zinatoa kinga ya kutosha. Hivyo aliwataka Watanzania wenye mitaji kuchangamkia fursa hii kutokana na uhakika wa soko uliopo katika sekta ya madini.

About The Author

error: Content is protected !!