KESI zilizofunguliwa na wanachama wa ACT Wazalendo wanaopinga matokeo ya uchaguzi wa uwakilishi Zanzibar, zimeingia katika mtihani mpya, safari hii pia ukitokana na “pingamizi” lililowekwa ndani ya usikilizaji ombi lao kabla ya malalamiko yao ya msingi kuanza kusikilizwa. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Kupitia jopo la wanasheria walio chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, upande huo umewasilisha pingamizi mpya leo mbele ya Jaji Salma Ali Hassan, aliyetarajiwa kuiongoza Mahkama Kuu katika kusikiliza ombi la zuio la uteketezaji wa nyaraka za uchaguzi uliopita.
Mwanasheria mwandamizi serikalini Said Salim Said alieleza mahkama kuwa wanashida na uhalali wa viapo vilivyoambatana na malalamiko ya waombaji. Kwamba wanaona havikuandaliwa na wakili mwenye leseni ya kuwa kamishna wa viapo.
Akadai kuwa yawezekana anayo leseni halali ya uwakili Zanzibar, hofu yetu hajapata kibali cha kuwa msimamizi wa viapo katika kesi zinazofunguliwa kwenye Mahkama Kuu. “Hapa Zanzibar, tofauti na kule Bara, ukishakuwa wakili huwezi kuwa hapohapo msimamizi wa viapo vikatumika kufungua kesi, mpaka upate kibali cha kisheria,” alieleza.
Sasa, anadai, huyu wakili, akimtaja kwa jina lake Ussi Khamis Haji, aliyeshuhudia viapo katika kesi hizi, aliridhia na kusaini viapo. Tunachofahamu ni kwamba “anataka kuaminisha jamii na wateja wake, kwamba wakati akifanya haya, ana leseni halali kumbe si kweli.”
“Wakili hapa Zanzibar aweza kuwa na leseni akashughulikia kuwakilisha wateja mahkamani, lakini asiwe msimamiaji viapo. Hana leseni ya kuwa kamishna wa viapo, leseni inaishi kwa mwaka mmoja ukikoma inatakiwa upate mpya.
“Tunamfahamu wakili Ussi Khamis Haji amekuwa akisimamia viapo bila ya kuwa na leseni husika. Utafiti wetu kupitia chanzo thabiti umebaini hajapata leseni mpya ya kuwa kamishna wa viapo,” alidai mahkamani.
Mwanasheria Said alieleza kuwa anayo barua ya tarehe 18 Disemba 2025 ya Mrajis {Msajili} wa Mahkama Kuu inayoonesha uhalali wa leseni aliyonayo Wakili Ussi.
“Hajapata leseni mpya {mwaka huu},” aliambia Mahkama iliyojaa wasikilizaji.
Lakini mwanasheria huyo alipotaka kuitumia kama kielelezo barua alotaja ni ya tarehe 10 Februari 2026 iloandikwa na Mrajis ikizungumzia hadhi ya ukamishna wa viapo ya Wakili Ussi, aliibuka Wakili Rajab Abdalla Rajab, anayewakilisha walalamikaji, akainuka na kumtanabahisha Jaji Salma.
Wakili Rajab alieleza kuwa haikubaliki. “Tunakataa kupokewa barua hii, kwa sababu haiwezi kuthibitisha hayo. Na tunakopelekwa itatulazimu kutanua wigo na kutaka nasi tufanye uchunguzi wa hayo na huko ni mbali kusikohusu kwa hatua tuliopo,” alieleza.
Wakili Rajab alieleza kwamba kukubali wanavyotaka walalamikiwa, kutakuwa na maana ya kumtaka mwenyewe atoe ushahidi. “Hii itakuwa ni ombi la kushtukiziana,” alidai.
Hoja yake ilitokana na kile alichodai suala hilo ni geni kwao, halikuwa kwenye majibu ya walalamikiwa, ni jana tu ndio liliwafikia upande wao katika kipindi ambacho “sote tunajua tumekuja kusikiliza ombi la zuio la mahkama kuhusu uteketezaji nyaraka za uchaguzi.”
Maelezo hayo ya Wakili Rajab yalisababisha tafakuri upande wa Jaji Salma. Dakika chache baada ya kurudia kumbukumbu zake, aliamua kuakhirisha kesi kwa nusu saa. Baadaye wasikilizaji walijulishwa na karani wa Jaji Salma kuwa mahkama itarudi ifikapo Saa 7 mchana. Wakati huo ilikuwa ni Saa 5:32.
Mahkama iliporejea, ikiwa ni Saa 7:16 mchana, Jaji Salma alisema ameamua hapokei barua ya upande wa walalamikiwa, na sababu angezitoa baadaye kadiri inavyoendelea. Akaelekeza mwanasheria Said aendelee na maelezo yake.
Akaeleza kuwa ndivyo imani yao ilivyo kuwa Wakili Ussi hakuwa na leseni ya ukamishna wa viapo wakati akiandaa kesi za walalamikaji. Kwa hivyo, ni maoni yao kuwa mahkama ijiridhishe na hilo huku ikielewa ni utaratibu uliozoeleka mahkama kuzuia wakili asiyekuwa na leseni.
Akataja rufaa iliyoamuliwa na Mahkama ya Rufaa Tanzania aliposikilizwa Edson Ndunguru dhidi ya Emmanuel Nchimbi {sasa Makamu wa Rais}, na mwenzake. Ukurasa wa 12 na 13 wa uamuzi unaeleza kuwa ombi linakosa uhalali wa kisheria ikiwa limeandaliwa na wakili asiyekuwa na leseni husika.
“Kesi iliopo mbele yetu Mhe Jaji inakwenda mbali ya hapo. Tunaomba sasa utupilie mbali ombi lao hili. Tuna maana kuwa ombi mbele yako halina kiapo halali, kwa maana pana ombi lenyewe halina uhalali wa kisheria, hakuna ombi halali,” alieleza.
Ndipo Jaji Salma, baada ya kusikia upande wa walalamikaji kuhusu hilo, wakieleza kuwa hawana cha kueleza kusonga mbele kwa hoja hiyo, alipoamua kupanga tarehe 13 Februari, Ijumaa, kuja kutoa uamuzi.
Pingamizi la kuhoji uhalali wa wakili aliyesimamia viapo vya waliofungua malalamiko ya matokeo ya uchaguzi, limekuja ghafla kwa kuwa leo ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza shauri la kudai zuio la kuteketeza nyaraka za uchaguzi kufuatia tamko la tarehe 3 Februari la Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} kuidhinisha kuteketezwa nyaraka za uchaguzi unaolalamikiwa.
Akitoa tamko hilo, Mwenyekiti wa Tume, Jaji George Kazi, alisikika akisema tume imeidhinisha zoezi hilo kwa mujibu wa kifungu 98(3) kinachotoa ruhusa ikiwa hakuna zuio la kisheria. Tamko hilo liliibua kauli yenye matamshi makali upande wa ACT Wazalendo, ikidai Tume inakusudia kufuta ushahidi wa kesi zilizofunguliwa kupinga matokeo ya uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti Ismail Jussa Ladhu alisema ni fedheha Tume kujificha chini ya kivuli cha kifungu cha sheria huku yenyewe ikiwa imejibu malalamiko yaliyowasilishwa na wagombea kuwa itatumia nyaraka za uchaguzi katika ushahidi wake.
Jussa aliyezungumza na waandishi wa habari tarehe 6 Februari, Vuga mjini Zanzibar, alisema hicho kifungu hakilazimishi Tume kuharibu nyaraka; isitoshe haijawahi kutokea zoezi hilo kufanywa kwa matangazo na likafanywa mara tu siku zenyewe 90 kutimia.
“Tunawaambia Tume watambue kwamba kufuta au kuharibu ushahidi wa kesi ilioko mahkamani ni kosa la jinai. Hatuoni busara ya hii tume inayoongozwa na majaji kufanya kitendo hichi cha kuvunja sheria,” alisema.
Akataja mambo matatu yazingatiwe kuhusu nyaraka za uchaguzi; Kwanza, zoezi la kuteketeza nyaraka lisitishwe; pili, Mahkama Kuu isikilize ombi la walalamikaji {ACT} kuhusu kuruhusiwa kukagua na kupekua nyaraka za uchaguzi; na tatu, vyombo husika vya ulinzi na usalama vidhibiti, kuhifadhi na kulinda nyaraka zote zinazohusu uchaguzi uliopita mpaka pale mashauri yaliyoko mahkamani yamalizike.
Chama hicho kilikimbilia mahkamani kufungua shauri na kuambatanisha na hati ya dharura kikitaka amri ya muda ya kusimamisha uteketezaji wa nyaraka za uchaguzi wa 2026. Mahkama kupitia Jaji Salma baada ya kusikiliza hoja za upande mmoja, ilitoa amri ya muda.
Alipanga tarehe 10 leo kusikiliza shauri ambako upande wa walalamikiwa ungepata nafasi ya kusikilizwa. Mbali na Tume ya Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ndiye mlalamikiwa katika kesi zilizofunguliwa kupinga matokeo ya uchaguzi. Kesi 25 zimefunguliwa, 17 zikiwa za majimbo ya Unguja na nane majimbo ya kisiwani Pemba.
ZINAZOFANANA
TAMISA yataja maeneo 20 muhimu ya ‘kupiga pesa’ kwenye madini
Niandike,niseme nini kuhusu Lowassa?
Lissu alalamika kuchelewa kesi yake