Tundu Lissu akiingia mahakamani
BAADA ya kesi inayomkabili mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (TL), kughairishwa kwa siku 88, hatimaye leo Jumatatu, tarehe 9 Februari 2026, mwanasiasa huyo ametinga tena mahakamani. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Mbele ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Lissu anayekabiliwa kesi ya uhaini, Na. 19605/2025, amelakiwa na mamia ya wanachama, viongozi na wafuasi wa chama chake.
Aliwasili mahakamani, majira ya saa 2:32 asubuhi, akionekana kuwa na afya njema; ari na nguvu ya kukabiliana na kesi yake.
Kesi dhidi ya Lissu, ilifunguliwa tarehe 10 Aprili mwaka 2015. Inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kabla ya kesi kuhairishwa kwa kesi yake, tarehe 12 Novemba mwaka jana, Lissu aliibua pingamizi la uhalali wa kutumika kwa sheria ya kulinda mashahidi.
Alisema, sheria hiyo haijachapishwa kwenye Gazeti la Serikali (Government Gazette) na kwamba sheria yoyote ambayo haijachapishwa kwenye Gazeti la Serikali, haiwezi kutumika.
Lissu aliibua pingamizi hilo, wakati Serikali ikimleta mahakamani, shahidi wake wa nne, aliyepewa jina la siri la ‘P1,’ ili kuanza kutoa ushahidi.
Mwanasiasa na mwanasheria huyo machachari nchini, aliiambia mahakama kuwa hata kama sheria ya ulinzi wa mashahidi ingekuwa halali kutumika, basi shahidi huyo alitakiwa kuonwa na majaji.
Aliongeza, “Lakini hata majaji wanaoendesha shauri hili, hawawezi kumuona shahidi aliyepo mbele yao na ambaye anataka kutoa ushahidi kwenye kesi nzito yenye hukumu ya kifo. Hili siyo jambo linalokubalika kwa mujibu wa sheria zetu,” alifafanua.

Kwa mujibu wa tararibu za mahakama, leo inatarajiwa Jamhuri kuanza kujibu hoja za mtuhumiwa, huku chama chake, kikitoa wito kwa umma, kufuatilia kwa umakini muendelezo wa kesi hii, wakiitaja kuwa yenye taswira muhimu ya demokrasia na haki nchini Tanzania.
Nje na ndani ya viunga vya Mahakama Kuu, mamia ya wananchi wamefurika kufuatia kesi ya kiongozi huyo, aliyejipambanua katika kutetea utawala wa sheria, haki za binadamu na demokrasia.
ZINAZOFANANA
Lissu alalamika kuchelewa kesi yake
Tuzo za ZICA: NBC yaibuka kinara uwezeshaji miradi ya ujenzi Zanzibar
Serikali kujibu hoja za Lissu, kumpinga shahidi wa siri kesho