February 3, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

RITA kuwanoa wajumbe Bodi za wadhamini mikoa sita

 

KUONGEZEKA kwa matukio ya ubadhirifu, migogoro na usimamizi usioridhisha katika baadhi ya taasisi za kidini, vyama vya michezo na asasi za kiraia, Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA imeandaa mkutano na mafunzo kwa wajumbe wa Bodi za Wadhamini katika mikoa sita ilikuwajengea uwezo zaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi Frank, amesema pamoja na mengine washiriki watapata mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa eRITA unaotumika katika usimamizi na uwasilishaji wa taarifa kwa njia salama na ya haraka.

“Mkutano huo utakaofanyika tarehe 11 na 12 mwezi huu mkoani Katavi na utawashirikisha pia wajumbe kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya na Songwe,” amesema Kanyus na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao wakizingatia sheria, kanuni, taratibu sambamba na kusimamia katiba za taasisi zao.

Kanyuai ameongeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera na unatarajiwa kuwa na washiriki wapatao 500 ambao ni wajumbe wa Bodi za Wadhamini pamoja na wadau mbalimbali wa Usajili wa Bodi za Wadhamini.

“Mpaka sasa Wajumbe wa Bodi za Wadhamini wapatao 1200 tayari wameshapata elimu katika mikoa sita. Tuameamua kutoa elimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wadhamnini kufuatia kuongezeka kwa matukio ya usimamizi usioridhisha katika baadhi ya taasisi, hali inayosababisha matumizi mabaya ya fedha, migogoro isiyoisha, na kuvuruga utendaji wa kawaida wa taasisi hizo’’ amesema Kanyusi.

RITA, pamoja na majukumu mengine, imepewa mamlaka kisheria ya kusajili na kusimamia Bodi za Wadhamini kwa mujibu wa sheria ya usajili wa bodi za wadhamini sura ya 318 na imekuwa ikiandaa Mafunzo kwa wadhamini ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu hasa katika eneo la usimamizi wa mali na rasilimali za taasisi wanazozisimamia.

Afisa Mtendaji Mkuu huyu, ametoa wito kwa wajumbe wa Bodi za wadhamini katika mikoa itakayoshiriki mkutano huo kujisajili kupitia namba za simu zinazopatikana katika Tovuti na akaunti za mitandao ya kijamii za Wakala pamoja na matangazo yanayorushwa katika vyombo vya habari.

About The Author

error: Content is protected !!