Geoffrey Mwambe
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeahirisha kusikiliza maombi Na. 488/2026 yaliyofunguliwa na Waziri wa zamani, Geoffrey Mwambe dhidi ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) hadi Jumatatu ya tarehe 26 Januari 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa leo tarehe 23 Januari 2026, imeahirishwa kufuatia ombi la upande wa Jamhuri uliowasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daniel Nyakia, aliyedai kutokuwepo kwa mashahidi wawili muhimu waliotajwa kwenye kiapo cha mleta maombi.
Mashahidi hao ni maafisa wa Uhamiaji, mmoja akitokea Sirari mkoani Mara na mwingine Namanga mkoani Arusha, ambao kwa mujibu wa upande wa Jamhuri ni wadau muhimu katika maombi hayo.
Wakili Nyakia alieleza kuwa hadi wanawasili mahakamani hapo leo, hawakuwa wamefanikiwa kuwapata maafisa hao kwa wakati, hivyo kuiomba mahakama isogeze mbele usikilizwaji wa kesi hiyo ili kutoa nafasi ya kuwasiliana nao na kuwasilisha kiapo kinzani.
Baada ya mjadala wa muda mfupi kati ya mawakili wa pande zote, akiwemo Wakili Mwandamizi, Mpale Mpoki kwa upande wa mleta maombi, Mahakama ilikubaliana na ombi la Jamhuri.
Hatimaye, Mahakama iliagiza upande wa Jamhuri kuhakikisha wanawasilisha kiapo kinzani kabla au ifikapo asubuhi ya Jumatatu,ya 26 Januari 2026, na kwamba kesi hiyo itasikilizwa siku hiyohiyo saa 8:30 mchana.
ZINAZOFANANA
Chadema: Muda wa zuio la kufanya shughuli za siasa umekwisha
NBC yaahidi kuimarisha ushirikiano na wadau, yasisitiza mwelekeo wake
Tundu Lissu asherehekea Birthday gerezani