February 2, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Hesabu zakataa ushindi wa CCM

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele

 

MJADALA wa ushindi wa asilimia 97 ya kura zilizotangazwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025, bado ungali mbichi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI wiki hii, Dk. Richard Mbunda, mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameeleza kuwa “Idadi ya watu waliopiga kura, haiendani na uhalisia.

Amesema, “Watu 32,678,444 walipiga kura, hawalingani na uhalisia. Vituo vilikuwa 99,911, ukivigawa na idadi ya wapiga kura wote unapata wastani wa wapiga kura 377 kwa kila kituo.

“Muda wa kupiga kura ni saa tisa, sawa na dakika 540, tuchukulie kila mpiga kura mmoja atatumia dakika mbili. Kwa  kufuata mchakato wa kupiga kura kwa muda wa saa tisa, watakaoweza kupiga kura, ni watu 270 huku watu 100 wakiwa wanasubiri. Lakini tumeambiwa watu hao wote walipiga kura kwa saa tano tu, hizi hesabu zinakinzana na uhalisia,” ameeleza.

Amesema, namba zinagoma kushabihiana na matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi (INEC).

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele, alimtangaza Rais Samia, kupata kura 31.9 milioni, sawa na asilimia 97.66 ya kura zote zilizopigwa.

Kauli ya Dk. Mbunda imekuja wiki moja baada ya waziri mkuu mstaafu,Joseph Warioba, kushangazwa na ushindi huo na idadi ya watu waliotajwa kujitokeza kupiga kura.

Alisema, “Hakuna uhalisia kwa kuwa kwenye vituo kulikuwa na idadi ndogo ya watu na baadhi ya maeneo kuibuka vurugu, kabla ya zoezi la uchaguzi halijakamilika.”

Aidha, baadhi ya wachambuzi wanasema, kwa takriban siku nne, mtandao ulizimwa hivyo haikuwa rahisi kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kutuma matokeo kama inavyofanyika katika chaguzi zilizopita.

Dk. Mbunda amesema, mchakato wa uchaguzi a umeonyesha kuna kasoro kwenye Katiba.

Anasema, “Uchaguzi ulioisha tumesikia ukitajwa kuwa haukuwa huru wala haki na haukidhi viwango vya uchaguzi vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Rais Samia Suluhu Hassan

Amesema, takwimu za matokeo ya uchaguzi huo zinatia shaka kwa kuwa haziendeni na uhalisia.

“…watu milioni 32 waliwezaje kupiga kura katika kipindi kifupi na wakawa wamemaliza,” anahoji Dk. Mbunda na kuongeza, “Ndio maana watu wanatilia shaka kilichotangazwa.

Anasema, wananchi hawakuona misururu ya watu waliojitokeza kupiga kura, kwa hiyo hesabu inaonesha dhahiri kwamba  hesabu inagoma.

Naye PrayGod Sallema, Mchambuzi wa masuala siasa nchini amesema, Chama Cha Mapinduzi, kimelazimisha mtokeo bila kupiga hesabu vizuri.

“Kuna msemo wa wahenga unasemao, kufa kwa nyani miti yote huteleza. CCM wanafanya ulazima wa kutafuta uhalali katika uchaguzi wa 29 Oktoba. Lakini ukweli ni kwamba wanachokieleza, hakuna anayeweza kukiamini,” amefafanua.

Alisema, hajapata kusikia uchaguzi unaompa ushindi wa asilimia 97 kwa mgombea urais ndiyo maana hivi sasa viongozi wanahaha kuweka mambo sawa mbele ya jumuiya za kimataifa.

“Hata nchi ya chama kimoja kuna kura za hapana na zile za watu kutopiga kura, lakini hazifiki asilimia 97 tunawasiwasi walioshauri jambo hili hawakuwa wamefanya utafiti vizuri kwenye hili,” ameeleza.

Amesema, katika kulazimisha walichokitaka ‘ushindi wa kishindo’ wamemfanya Mzee Warioba, kutoka hadharani na kueleza uhalisia.

 “Huyu (Jaji Warioba), ndio mzee pekee anayeaminika katika wazee waliosalia katika taifa hili na bado anasimama upende wa ukweli na wa haki tunao wazee wengi walishika nyadhifa mbalimbali lakini hawasemi chochote.”

Naye Makame Kidegwade, mkazi wa Ilala Dar es Salaam, ameeleza kuwa kujitokeza kwa Jaji Warioba kumekata mzizi wa fitna kwa kuwa ameeleza kile ambacho wananchi walikuwa wanakitilia shaka.

“Hakuishia kuonesha udhaifu, ameonesha pia mahali pa kuanzia ili taifa lijinasue kwenye mgogoro ulioibuka,” amesisitiza.

Aliyekuwa mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara ‘Bwege,’ amesema kwa namna alivyomsikia Jaji Warioba, “ameibuka kama mpatanishi wa taifa.

 “Ni mzalendo yeye hajali kutukanwa wala kupigwa yeye ni Tanzania kwanza ni mzalendo kwali kweli mimi naweza kumuita Mildfield kiungo muunganishaji.”

About The Author

error: Content is protected !!