Kapteni Ibrahim Traore, kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso
KAMPTENI Ibrahim Traore, kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, amenusurika kuuliwa. Serikali ya taifa hilo la Afrika Magharibi, imetangaza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa serikali, mpango huo ulikuwa uliratibiwa na Luteni Kanali Paul Henri Damiba, afisa wa kijeshi aliyeondolewa madarakani na Traore mwezi Septemba 2022.
Katika taarifa yake ya usiku wa manane, waziri wa usalama wa ndani alisema, shirika la kijasusi la Bukinafaso, limezuia operesheni hii katika saa za mwisho.
“Walikuwa wamepanga kumuua mkuu wa nchi na kisha kushambulia taasisi zingine muhimu, wakiwemo watu mashuhuri,” amesema Mahamadou Sana, akidai njama hiyo imeandaliwa nchi jirani ya Ivory Coast.
Hakuna taarifa yoyote kutoka kwa Kanali Damiba au Ivory Coast kunakodaiwa kupangwa mkakati huo.
Tangu alipochukua madaraka, Kapteni Traoré amekabiliwa na majaribio mawili ya mapinduzi na pia anakabiliwa na ongezeko la vurugu za wanajihadi ambazo zimewalazimisha mamilioni ya wananchi wa taifa hilo, kukimbia makazi yao.
Jaribio la karibuni kabisa lilikuwa Aprili mwaka jana, ambapo serikali ya kijeshi ilisema imezuia “njama kubwa” ya kumpindua kiongozi wake.

Serikali ya Kapteni Traoré, ilidai kuwa wapanga njama hao walikuwa wakifanya kazi kutoka nchi jirani ya Ivory Coast.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema kuwa jaribio hilo la mapinduzi liliongozwa na wanajeshi wa sasa na wa zamani waliokuwa wakishirikiana na viongozi wa makundi ya kigaidi.
Alisema kuwa mpango wao ulikuwa kushambulia Ikulu ya rais wiki iliyopita.
Lengo kuu, alisema, lilikuwa “kusababisha vurugu kubwa na kuiweka nchi chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa.” Alitoa kauli hiyo kupitia televisheni ya taifa.
Licha ya changamoto hizi, kiongozi huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 37 ana uungwaji mkono mkubwa na amepata wafuasi kote Afrika kwa maono yake ya umajumui wa Kiafrika na ukosoaji wake wa nchi za Magharibi.
Kulingana na waziri wa usalama, serikali iligundua video iliyovuja ikiwaonyesha wapangaji wakijadili mipango yao.
Katika picha hizo, inadaiwa walizungumzia jinsi walivyokusudia kumuua rais – iwe karibu au kwa kuweka vilipuzi nyumbani kwake, Jumamosi ya 3 Januari.
Baadaye inadaiwa walipanga kuwalenga maafisa wengine wakuu wa kijeshi na raia.
Sana amedai Damiba amekusanya wanajeshi na wafuasi wa kiraia, akapata ufadhili wa kigeni – zaidi ya faranga 70 milioni za CFA ($125,000; £92,000) zilizotolewa kutoka Ivory Coast – na alipanga kuangamiza kambi ya ndege zisizo na rubani nchini humo kabla ya vikosi vya kigeni kuingilia kati.
“Tunafanya uchunguzi na tumewakamata watu kadhaa. Watu hawa watafikishwa mahakamani hivi karibuni,” ameeleza waziri huyo.
Haijulikani ni watu wangapi wamekamatwa.
Kanali Damiba alihudumu kama kiongozi wa Burkina Faso kuanzia Januari hadi Septemba 2022 baada ya kunyakua madaraka kutoka kwa serikali iliyochaguliwa kiraia.
Baada ya kufukuzwa alikwenda uhamishoni katika nchi jirani ya Togo na akasema katika ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba anamtakia mrithi wake kila la heri.
ZINAZOFANANA
Kujiondoa kwa mtoto Mbowe Chaumma, kuna maanisha nini?
Hesabu zakataa ushindi wa CCM
Watu 100 wameuawawa shambulio la kukamatwa Maduro